Sep 10, 2023 10:55 UTC
  • Iran yasikitishwa na zilzala iliyoua maelfu Morocco; kutuma nchini humo misaada ya kibinadamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kutuma misaada ya kibinadamu nchini Morocco, kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoua maelfu ya watu.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kusisitiza kuwa, Iran itatumia suhula zake zote kuisaidia na kuihudumia serikali na wananchi wa Morocco katika mazingira haya magumu baada ya zilzala.

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Morocco kufuatia tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha rishta.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesikitishwa na kuhuzunishwa na vifo vya maelfu ya watu kutokana na zilzala hiyo.

Amir-Abdollahian amesisitiza katika ujumbe wake huo aliouandika kwa lugha ya Kiarabu kuwa, mashirika ya kutoa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu yako tayari kutuma misaada ya dharura huko Morocco.

Ameongeza kuwa, Shirika la Hilali Nyekundu la Iran liko tayari kuisaidia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika operesheni za uokozi na kuwashughulikia majeruhi na waathiriwa wa zilzala hiyo.

Mtetemeko huo wa ardhi uliotokea usiku wa kuamkia Jumamosi ya jana umepelekea zaidi ya watu 3,000 kupoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa. Mfalme Mohammed VI wa Morocco ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kuamuru kupelekwa misaada ya chakula na misaada kwa walionusurika.

Tags