Iran yazionya Marekani na Israel juu ya 'matokeo hasi makali' endapo jinai za kivita zitaendelea Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amezionya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba zitakabiliwa na "matokeo hasi makali" iwapo zitashindwa kukomesha kikamilifu uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza uliofanywa wakati wa vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya eneo Palestina lililowekewa mzingiro.
Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mahojiano na chaneli ya televisheni wa Al Jazeera ya Qatar yaliyochapishwa leo Jumanne, huku kukiwa na mapatano ya muda ya usitishaji vita huko Gaza ya utawala wa Kizayuni na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonya kwa kusema: "ni muhimu kwamba uchokozi na uhalifu [wa Israel] lazima ukomeshwe na usitishaji vita wa muda lazima uwe wa kudumu. Vinginevyo, eneo litashuhudia hali nyingine mpya".
Ameongezea kwa kusema: "utawala wa Kizayuni na Wamarekani itawapasa wakubali matokeo hasi makali ya kushindwa kukomesha uhalifu wa kivita".
Usitishaji vita wa siku nne katika Ukanda wa Gaza uliomalizika jana Jumatatu, umerefushwa kwa siku mbili zaidi na kupelekea kusimamishwa vita angamizi vilivyoanzishwa na utawala katili wa Israel dhidi ya eneo hilo la Palestina na kufanyika zoezi la kuachiwa huru Wapalestina waliokuwa wakiteseka na kuatilika ndani ya magereza ya Israel na mateka wanaoshikiliwa na harakati ya Hamas.
Katika mahojiano hayo na Aljazeera, Amir-Abdollahian ameendelea kueleza kwamba, Israel inakaribisha kuendelea na kupanuka kwa vita endapo Marekani itaendelea kuunga mkono kikamilifu mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.
Ameongezea kwa kusema, Tehran imearifiwa kupitia duru za ubadilishanaji wa taarifa kwamba Ikulu ya White House hivi karibuni imegundua kwamba kuendelea kwao kuiunga mkono Israel si kwa manufaa yake.
Mwanadiplomasia mkuu wa Iran amebainisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel umeshindwa kuiangamiza Hamas katika kipindi cha wiki sita zilizopita licha ya kupata msaada na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na nchi washirika wa Washington.
Amir-Abdollahian amesisitiza kwa kusema: "Hamas ni uhakika uliojikita na kutoa mizizi ndani ya Palestina. Hamas ni sehemu ya Muqawama wa Wapalestina, na tunaamini kwamba mustakabali wa Gaza utaamuliwa na watu wa Palestina na Muqawama"…/