Dec 21, 2023 03:28 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran azungumza na waziri mwenzake wa Afrika Kusini, Ghaza maudhui kuu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Afrika Kusini na kujadiliana naye masuala mbalimbali muhimu ya pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa na hasa vita vya Ghaza huko Palestina.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo hayo ya simu na Bi Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini na sambamba na kuelezea kufurahishwa kwake na jinsi uhusiano wa pande mbili unavyozidi kustawi na kuimarika amesema kuwa, anaishukuru Afrika Kusini kwa msimamo wake imara na madhubuti wa kuwatetea wananchi madhlumu wa Palestina.

Vile vile ametilia mkazo wajibu wa kuendelezwa jitihada za pamoja katika nyuga za kimataifa za kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na kuchukuliwa hatua za kivitendo za kukomeshwa vita huko Ghaza pamoja na kupunguziwa mateso wananchi wa Palestina wanaodhulumiwa kila upande, kila sekunde na kwa makumi ya miaka na utawala katili wa Kizayuni. 

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina hazina mfano katika historia

 

Kwa upnde wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msimamo wake imara na kwa jitihada zake kubwa za kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kusema kuwa nchi hizi mbili zina wajibu wa kuendeleza ushirikiano wao katika kupigania kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na maeneo mengine ya Palestina.

Amesema: Kwa bahari nzuri msimamo rasmi wa serikali ya Afrika Kusini unakubaliana na fikra na mtazamo wa wananchi wa nchi hiyo katika kadhia nzima ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kupinga jinai za utawala wa Kizayuni na hilo limepelekea serikali ya nchi hiyo kuiandikia barua rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ikiitaka mahakama hiyo kufuatilia jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wala hatia wa Palestina.

Tags