Feb 06, 2024 03:00 UTC
  • Rais Raisi: Sera ya msingi ya Iran ni kuunga mkono nchi zinazojitenga na Israel

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema sera ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuunga mkono nchi zinazojitenga na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Raisi ameyasema hayo katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali al-Sadiq Ali mjini Tehran siku ya Jumatatu ambapo ameongeza kuwa: "Upuuzaji wa baadhi ya nchi za Kiislamu kuhusu sera hii ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umetoa pigo kubwa kwa Umma wa Kiislamu."

Ameongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel daima umekuwa ukipanga njama za kukwamisha njia ya nchi za Kiislamu kuelekea maendeleo na ustawi.

Israel haitakuwa rafiki wa nchi za Kiislamu wala haipendezwi na maendeleo ya nchi hizo, alisisitiza.

Rais wa Iran alikosoa hatua ya baadhi ya tawala nchi za Kiislamu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, hatua ambayo inaenda  kinyume na matakwa ya kiasili ya mataifa.

Halikadhalika amesema: "Lau nchi hizi zingejaribu kukata uhusiano wao na Wazayuni, leo hii tusingeshuhudia kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu dhidi ya watu wanaodhulumiwa na Waislamu wa Ghaza."

Nchi nne za Kiarabu - Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco - zilikubali kuanzisha uhusiano na Israel chini ya makubaliano yaliyopitishwa na Marekani mwaka 2020, wakati Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipokuwa madarakani.

Hatua hiyo ililaaniwa vikali na Wapalestina pamoja na mataifa mengi na watetezi wa haki za binadamu kote ulimwenguni, haswa ndani ya ulimwengu wa Kiislamu.

Wapalestina wanaona mapatano hayo kama usaliti katika mapambano ya kukomboa ardhi yao kutoka kwa makucha ya utawala haramu wa Israel.

Hossein Amir Abdollahian (kulia) katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Al-Sadiq Ali, Tehran Feb 5 2024

Kwingineko katika matamshi yake, Raesi alisema Iran inaunga mkono kikamilifu mamlaka ya kujitawala Sudan na kuanzishwa kwa serikali yenye nguvu katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Pia alikaribisha ufufuo wa mahusiano ya pande zote baada ya miaka saba ya kukatwa.

Akiashiria uwezo na azma za nchi hizo mbili za kukuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ameongeza kuwa, kubadilishana mabalozi na kufunguliwa tena balozi Tehran na Khartoum kutatayarisha uwanja mwafaka wa kuimarishwa uhusiano.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Sudan amesema nchi yake ina nia ya kurejesha uhusiano wake wa kisiasa na kidiplomasia na Iran.

Amepongeza uungaji mkono wa kisiasa wa Iran kwa Sudan katika duru za kimataifa na kusema Khartoum iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Tehran.

 

Tags