Mar 25, 2024 02:51 UTC
  • Wairani waandamana kulaani jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Wananchi wa Iran wamefanya maandamano makubwa katika sehemu mbalimbali za nchi ukiwemo mji mkuu Tehran, kutangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina wanaoendelea kuuawa, sambamba na kulaani jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran ya Kiislamu jana usiku walifanya maandamano wakieleza masikitiko yao kwa jinai zinazoendelea kufanywa na Wazayuni huko Gaza, sambamba na kutangaza chuki na hasira zao kutokana na uovu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Hapa jijini Tehran, kundi la waandamanaji wakiwemo wanafunzi wa Vyuo Vikuu lilikusanyika nje ya ubalozi wa Uingereza kulaani umwagaji damu unaoendelea kufanywa na Wazayuni maghasibu huko Gaza kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi.

Kundi jingine la waandamanaji hapa Tehran lilikusanyika katika Medani ya Palestina, huku waandamanaji wengine wakipiga nara dhidi ya Wazayuni na waungaji mkono wao Wamagharibi katika Msikiti Mkuu wa Imam Khomeini na wengine wakiandamana katika Msikiti wa Arg.

Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, waandamaji hao wamekosoa vikali uvamizi na mzingiro dhidi ya Hospitali ya al-Shifa kwa siku ya kadhaa mfufulizo na kueleza kuwa, waungaji mkono na wale wanaonyamazia kimya jinai za kinyama na za kutisha za Wazayuni huko Gaza wanapasa kufedheheka.

Wanawake pia wameshiriki maandamano ya kuwatetea Wapalestina

Kadhalika wananchi wa Iran wamezitaka jumuiya za kimataifa kusitisha mauaji yanayofanywa na utawala haramu wa Israel na kuwahudumia watu waliopatwa na maafa wa Palestina huko katika Ukanda wa Gaza.

Wananchi wa Iran walioshiriki katika maandamano hayo ya usiku wa kuamkia leo wanasema inasikitisha kuwaona walimwengu wamenyamazia kimya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza.

Maandamano kama haya ya kulaani uhalifu unaofanywa na Israel kwa msaada na himaya ya baadhi ya nchi za Magharibi huko Gaza yamefayika pia katika miji ya Mashhad na Tabriz, ambapo waandamanaji wamelaani jinai za utawala katili wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza udharura wa kusitishwa mara moja uhalifu huo.

Tags