Iran yaonya baada ya Israel kutishia kushambulia ndege yake ya abiria
(last modified Sat, 15 Feb 2025 07:15:45 GMT )
Feb 15, 2025 07:15 UTC
  • Iran yaonya baada ya Israel kutishia kushambulia ndege yake ya abiria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei ameukosoa vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutishia kushambulia ndege ya abiria ya Iran iliyokuwa imebeba raia wa Lebanon.

Baghaei amevitaja vitisho hivyo vya Israeli kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na mamlaka na uhuru wa kujitawala Lebanon. Ameyataka mashirika husika ya kimataifa, likiwemo Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), kuchukua hatua za kisheria kukomesha mwenendo huo "hatari" wa Israel.

Hapo awali, Mojtaba Amani, Balozi wa Iran nchini Lebanon, alisema kuwa safari za ndege mbili za kila wiki kutoka Iran hadi Beirut zilikatishwa Alkhamisi, huku akiikosoa serikali ya Beirut kwa kujaribu kutafuta ndege mbadala kwa ajili ya abiria hao.

Waziri wa Uchukuzi wa Lebanon, akiwa chini ya mashinikizo ya Israel alitangaza kufuta safari hizo za ndege, kutokana na madai ya Tel Aviv kwamba ndege hizo zilikuwa zimebeba pesa za kuipelekea Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei

Hatua hiyo ya serikali ya Lebanon iliwafanya wasafiri wa Lebanon kukwama katika uwanja wa ndege wa Tehran. Awali utawala wa Israel ulitoa tishio la kimyakimya la kuzishambulia ndege za Iran zinazosafiri kuelekea Lebanon.

Kukataliwa kwa ndege za Iran kutua Lebanon kulizusha maandamano karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut.