Iran: Kona zote za Israel zinaweza kufikiwa na makombora yetu
Meja Jenerali Mohammad Ali Jafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, amesema maeneo yote ya ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel yanaweza kufikiwa na makombora ya Jamhuri ya Kiislamu.
Akiongea hapo jana wakati wa duru ya mwisho ya mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Eqtedar-e-Velayat yaliyoshudia makombora ya balistiki yakirushwa kutoka katika maghala maalumu ya chini ya ardhi kote Iran, Meja Jenerali Jafari amesema kijiografia, makombora takriban yote ya nchi hii yanaweza kufika popote pale katika utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, chokochoko za maadui wa Iran ya Kiislamu zitakabiliwa na majibu makali. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, IRGC imesema mazoezi hayo yanalenga kuonyesha uwezo wa Iran wa kujihami na kuzuia adui sambamba na kuwa tayari jeshi lake kukabiliana na vitisho vyote dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na ardhi ya Iran. Kamanda Mkuu wa IRGC Meja Jenerali Mohammad Ali Jafari na mkuu wa kitengo cha anga za mbali katika IRGC Brigedia Jenerali Amirali Hajizadeh walisimamia luteka hiyo ya jana.
Mwezi Oktoba mwaka jana, Iran ilifanyia majaribio kombora la masafa marefu la balisitiki la Emad lenye uwezo wa kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa, jambo ambalo liliwakera sana wanasiasa wa Marekani na kutishia kuiwekea nchi hii vikwazo vipya.