Iran yakanusha madai ya kukubali mazungumzo kuhusu makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39117-iran_yakanusha_madai_ya_kukubali_mazungumzo_kuhusu_makombora
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la The Financial Times kuwa Tehran imekubali kuingia katika mazungumzo kuhusu mradi wake wa makombora.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 18, 2018 02:32 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kukubali mazungumzo kuhusu makombora

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekadhibisha ripoti iliyochapishwa kwenye gazeti la The Financial Times kuwa Tehran imekubali kuingia katika mazungumzo kuhusu mradi wake wa makombora.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, madai yaliyochapishwa na gazeti hilo hayana msingi na kwamba sera za Tehran kuhusu mpango wake wa makombora ziko wazi.

Amesisitiza kwamba makombora ya nchi hii ni kwa ajili ya malengo ya kiulinzi tu na wala hayana uhusiano wowote na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Gazeti la The Financial Times siku ya Jumanne lilinukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ujerumani, iliyodai kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Uingereza na Ufaransa pamoja na Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kufanya mazungumzo na maafisa wa Iran mjini Brussels, kuhusu mradi wa makombora wa Tehran pamoja na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo. 

Zarif na mawaziri wenzake wa Ulaya mjini Brussels

Qassemi amebainisha kuwa, kila mmoja anafahamu kuwa uwezo wa makombora wa Iran sio suala la kujadiliwa licha ya kampeni, vitisho na misimamo mikali ya Marekani na waitifaki wake dhidi ya makombora hayo.

Januari 11, Dakta Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran alikutana na kufanya kikao na Mogherini na mawaziri wenzake wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, na mazungumzo yao yalijikita kunako makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.