Boroujerdi: Hizbullah imechangia pakubwa kusambaratishwa ISIS
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetoa mchango mkubwa sana katika jitihada za kuangamizwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Alaeddin Boroujerdi aliyasema hayo jana katika mkutano wake na wanachama wa kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Ulaya mjini Brussels na kuongeza kuwa, Hizbullah ndio harakati mashuhuri zaidi ya kupambana na ugaidi Mashariki ya Kati.
Amesisitiza kuwa, nafasi athirifu ya Iran katika vita dhidi ya ugaidi katika nchi za Iraq na Syria ndio sababu kuu ya ghadhabu za Marekani na vitisho vyake vya kila mara vya vikwazo dhidi ya taifa hili.
Kadhalika katika mkutano huo wa masaa matatu, Alaeddin Boroujerdi amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Ulaya.
Huku akikosoa hatua ya Rais Donald Trump ya kuiondoa Marekani katika Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran amesema ushirikiano katika kadhia ya mabadiliko ya hali ya hewa kati ya Iran na EU ni uga ambao unapaswa kupatilizwa na mikakati inayofaa.
Kwengineko katika kikao hicho, Alaeddin Boroujerdi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Bunge la Iran amezikosoa nchi za Ulaya kwa kunyamazia kimya migogoro ya kibinadamu na kuuawa wanawake na watoto wadogo kwa silaha za Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinazouziwa Saudi Arabia, mkabala wa mamilioni ya dola.