Iran yalaani hujuma za kigaidi Pakistan na Iraq
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hujuma za hivi karibuni za kigaidi katika mji wa Lahore Pakistan na karibu na Baghdad mji mkuu wa Iraq.
Katika taarifa, Sadeq Hussein Jaber Ansari Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, oparesheni hizo mbili za kigaidi, moja katika bustani mjini Lahore na nyingine katika uwanja wa michezo mjini Baghdad ni ishara kuwa magaidi na wenye misimamo mikali hawawaonei huruma wanadamu wa kawaida na kwamba hakuna eneo lolote linalosalimika na uovu wao.
Jaberi Ansari amesema kukaririwa hujuma za kigaidi maeneo mbali mbali duniani ni jambo linaloashiria udharura wa kuchukuliwa hatua za haraka kimataifa ili kukabiliana na tatizo sugu la ugaidi na misimamo mikali.
Ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa magaidi wakufurishaji wa kundi la ISIS au Daesh walishambulia kwa bomu mechi ya soka katika uwanja mmoja mjini Iskanderiyah kusini mwa Baghdad na kupelekea watu wasiopungua 41 kupoteza maisha.
Aidha siku ya Jumapili watu 75 waliuawa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa kwenye mripuko katika mji wa Lahore, kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kundi la kigaidi la Taliban limedai kuhusika na hujuma hiyo iliyopelekea idadi kubwa ya watoto na wanawake kuuawa katika Bustani ya Gulshan Iqbal mjini humo.