Saudia inalenga kuvuruga uthabiti katika eneo
Mshauri wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, katika masuala ya kimataifa amesema Saudi Arabia inalenga kuvuruga uthabiti katika eneo kwa kuvuruga serikali zilizopo.
Hussein Amir Abdulahian aliyasema hayo Jumamosi usiku na kuongeza kuwa kuongezeka ugaidi kusini mwa Yemen hasa katika mji wa Aden ni moja ya matokeo ya hujuma ya Saudia nchini Yemen. Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita nchini Yemen, Mansour Haadi alilazimishwa na Saudia kujiuzulu ili Yemen ibakie bila serikali na hatimaye kuvuruga uthabiti wa nchi hiyo.
Ameashiria mapigano baina ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Umoja wa Famle za Kiarabu na Saudia Arabia mjini Aden na kusema UAE inataka kuonyesha uwezo wake na hatimaye ijitenge na muungano wa Saudia.

Amesema mapigano huko Aden yanaashiria kuwa kumekuwepo na hitilafu baina ya Saudia na Yemen lakini hazikuwa zinadhihirika wazi. Abdullahian amesema Saudia binafsi haina uwezo wa kaunzisha vita na migogoro katika eneo na kwamba nyuma ya pazia ni Marekani inayoendesha sera za kivita za Saudia nchini Yemen. Akiashiria mgogoro wa Syria, Abdullahian amesema vita vya Syria vilianzishwa kwa lengo la kuangamiza nchi zinazounga mkono mapambano ya Kiislamu na hatimaye kuimarisha nguvu za utawala wa Kizayuni lakini njama hizo zimefeli.