Rouhani: Pande zote zitajuta iwapo makubaliano ya nyuklia ya Iran yatavunjika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i41247-rouhani_pande_zote_zitajuta_iwapo_makubaliano_ya_nyuklia_ya_iran_yatavunjika
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pande zote husika zitajuta iwapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatasambaratika, katika hali ambayo Marekani inafanya jitihada za kuyafelisha mapatano hayo na kutoa vitisho vya kujiondoa kwenye makubaliano hayo kila mara.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2018 23:26 UTC
  • Rouhani: Pande zote zitajuta iwapo makubaliano ya nyuklia ya Iran yatavunjika

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pande zote husika zitajuta iwapo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatasambaratika, katika hali ambayo Marekani inafanya jitihada za kuyafelisha mapatano hayo na kutoa vitisho vya kujiondoa kwenye makubaliano hayo kila mara.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje ya Ufaransa, Jean-Yves Le Drian aliyeko safari rasmi ya kikazi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa JCPOA inabakia hai, kwa shabaha ya kuimarisha usalama, uthabiti na ushirikiano katika eneo.

Amesema, "Bila shaka, sisi tuko tayari kwa senario yoyote ambayo haitakuwa na maslahi kwetu."

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kubakia hai mapatano hayo ya kihistoria kutatuma ujumbe mzito duniani  kwamba mazungumzo na diplomasia ndiyo machaguo bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro, huku akitahadharisha kuwa, kuvunjika kwa makubaliano hayo hakutakuwa na maana nyingine ghairi ya kuonyesha kuwa mazungumzo ya kisiasa ni kupoteza wakati.

Rais Rouhani na Waziri wa Mambo ya Nje ya Ufaransa, Jean-Yves Le Drian

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakuwa mshirika wa kwanza kuyakiuka makubaliano hayo kati ya Iran na nchi za Kundi la 5+1 ya Julai mwaka 2015, huku akiutaka upande wa pili kutekeleza wajibu wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema Paris iko makini kuhakikisha kuwa makubaliano ya JCPOA yanabaki hai na yanatekelezwa ipasavyo.

Amebainisha kuwa, ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimethibitisha kuwa Iran imeyatekeleza makubaliano hayo kikamilifu na kwa msingi huo, Ufaransa itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mapatano hayo hayavunjiki.