Abdollahian: Marekani imekasirishwa na kusambaratishwa magaidi wa Daesh nchini Syria
Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, kusambaratishwa magaidi wa Daesh (ISIS) nchini Syria kumeikasirisha sana Marekani na kwamba vitisho vinavyotolewa hivi sasa na Washington dhidi ya Damascus vina shabaha ya kuhamisha mazungumzo ya Astana na Sochi na kuyapelekea Vienna na Geneva kwa lengo la kudhamini malengo ya Marekani.
Hossein Amir Abdollahian amesema hayo alipohojiwa na shirika la habari la IRIB na kuongeza kuwa, hakuna mafanikio yoyote iliyoyapata Marekani katika madai yake ya kupambana na magaidi wa ISIS. Amesisitiza kuwa, Wamarekani hata wamekuwa wakiwasaidia viongozi wakubwa wa genge la Daesh kutoroka katika maeneo wanakozidiwa nguvu lakini jeshi na vikosi vya ulinzi vya Syria kwa kusaidiwa na Iran na Hizbullah ya Lebanon na msaada wa anga wa Russia vimefanikiwa kutoa pigo kubwa na kuwashinda magaidi wa ISIS, mafanikio ambayo hayaifurahishi hata kidogo Marekani.
Amesema, katika upande wa kisiasa pia, Wamarekani wameona kuwa wamepoteza ushawishi wao katika mazungumzo ya amani ya Syria baada ya mazungumzo yanayosimamiwa na Iran, Uturuki na Russia ya Astana na Sochi kupata mafanikio makubwa zaidi kuliko mazungumzo ya Geneva na Vienna yenye ushawishi wa Marekani, hivyo Washington imeamua kutoa mashinikizo ya kila upande ili kuhakikisha mazungumzo ya Astana na Sochi yanahamia Vienna na Geneva.
Amesema, serikali ya Syria ndiyo inayozidi kupata ushindi katika medani ya kupambana na magaidi hivyo kila mwenye akili timamu anatambua kuwa serikali ya Damascus haina haja kabisa ya kutumia silaha za kemikali, na ushahidi unaonesha kuwa madai yote yanayotolewa hayana uthibitisho wowote.
Aidha amesema, Wamarekani wanataka kuonesha kuwa wana nguvu kupitia kutupa makombora katika maeneo fulani fulani ya Syria lakini uhakika ni kuwa White House haina uwezo wa kuvumilia vita vipya nchini Syria.