Iran: Hatutafanya mazungumzo mengine ya nyuklia na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49690-iran_hatutafanya_mazungumzo_mengine_ya_nyuklia_na_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, licha ya Tehran kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), haitafanya mazungumzo mengine ya nyuklia na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2018 01:07 UTC
  • Iran: Hatutafanya mazungumzo mengine ya nyuklia na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, licha ya Tehran kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), haitafanya mazungumzo mengine ya nyuklia na Marekani.

Mohammad Javad Zarif ametoa sisitizo hilo katika kikao cha nne cha Mazungumzo ya Mediterania kinachofanyika mjini Rome, Italia kufuatia hatua zinazochukuliwa na Marekani za kutaka kuanzisha mazungumzo mapya ya nyuklia na Iran.

Dakta Zarif amebainisha kuwa: JCPOA ni makubaliano mazuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo tena na Marekani kuhusiana na shughuli zake za nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mazungumzo ya nyuklia yaliyochukua muda wa miaka 12 kati ya Jamhuri ya Kiislamu na madola sita makubwa duniani, matunda yake yakiwa ni makubaliano ya JCPOA na kubainisha kwamba: Sasa ni zamu ya Ulaya na wanachama wengine wa JCPOA kugharimika na kuwekeza kwa ajili ya usalama wa dunia.

Waziri Zarif (katikati) katika kikao cha Mazungumzo ya Mediterania mjini Rome, Italia

Zarif aidha ameashiria baadhi ya uadui unaofanywa dhidi ya wananchi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: Si kwa miaka 40 tu ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kwa muda wa miaka elfu saba Iran imekuwepo na itaendelea kudumu baada ya hapo pia.

Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia misaada na uungaji mkono wa Saudi Arabia na baadhi ya nchi nyingine za Mashariki ya Kati kwa Saddam, Daesh, Taliban na Jabahtu-Nusrah na kueleza kwamba nchi hizo ndizo zinazopaswa kubadilisha siasa na mienendo yao katika eneo.../