Iran yalaani shambulizi la kigaidi Vienna nchini Austria
-
Saeed Khatibzadeh
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amelaani shambulizi la kigaidi lililotokea nchini Austria na kusema kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na mizizi ya ugaidi.
Mapema leo Saeed Khatibzadeh ametuma salamu za rambiambi kwa serikali na familia za wahanga wa shambulizi hilo la kigaidi nchini Austria na kusema kuwa: Ugaidi katika sura zake zote unapaswa kulaaniwa, na tukio la jana usiku mjini Vienna limeonyesha tena kwamba, ugaidi na misimamo ya kufurutu ada havitambui mipaka ya nchi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa Kutumia chuki na uchochezi badala ya mantiki na busara vinatengeneza mazingira yasiyo salama ya kusambaa zaidi misimamo ya kuchupa mipaka na ukatili.
Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa jamii ya kimataifa kwa jili ya kupambana na mizizi ya ugaidi na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa sehemu ya juhudi hizo.
Watu wanne, akiwemo gaidi mmoja, wameuawa na wengine wasiopungua 15 kujeuhiwa katika shambulizi hilo lililolenga maeneo sita ya Jiji la Vienna.