Iran yasema UN, WHO zinapendelea tekolojia ya Markeani katika chanjo
Afisa wa ngazi za juu katika sekta ya afya nchini Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ina wasi wasi kuwa taasisi muhimu za dunia kama vile Umoja wa Mataifa (UN) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinapendelea teknolojia ya Marekani ambayo haijafanyiwa majaribio ya kutosha katika uga wa chanjo ya COVID-19 au corona.
Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres jana Jumatatu, Daktari Sayyid Alireza Marandi, Mwenyekiti wa Akademia ya Sayansi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taasisi hizo mbili za kimataifa zinazishinikiza nchi zingine zitumie chanjo za Marekani ambazo taathira zake hasi katika mwili wa mwandamu bado haijachunguzwa kisayansi. Daktari Marandi pia amelaani kimya cha taasisi za kimataifa hasa UN na WHO kuhusu vikwazo vya kidhalimu vya Marekani katika uga wa tiba.
Mwenyekiti wa Akademia ya Sayansi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mara kadhaa amesisitiza kuwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani na waitifaki wake Wamagharibi vimeizuia Iran kupata dawa na vifaa muhimu vya tiba na hivyo kukiuka haki zao za binadamu.
Daktari Marandi amemshangaa afisa wa ngazi za juu wa WHO Bruce Aylward ambaye akiashiria hatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kupiga marufuku chanjo za corona za Uingereza na Marekani amesema kadhia ya kirusi cha corona haipaswi kuchanganywa na siasa. Daktari Marandi amesema matamshi kama hayo yasiyo na busara yamepelekea kuwepo wasiwasi kuwa WHO inapendelea teknolojia ya Marekani ambayo haijafanyiwa majaribio ya kutosha na ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya wengi duniani. Amesema WHO imechukua muelekeo kama huo ili kuishawishi Marekani irejee WHO baada ya kujiondoa.
Siku ya Ijumaa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alitangaza bayana kuwa, kuingizwa chanjo ya COVID-19 kutoka Marekani na Uingereza nchini Iran ni marufuku.