Iran yazindua 'Jumba la Ubunifu na Teknolojia' Nairobi, Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66182-iran_yazindua_'jumba_la_ubunifu_na_teknolojia'_nairobi_kenya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuzinduliwa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Kenya na hata nchi nyingine za kanda ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2021 00:50 UTC
  • Iran yazindua 'Jumba la Ubunifu na Teknolojia' Nairobi, Kenya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuzinduliwa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya Iran na Kenya na hata nchi nyingine za kanda ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika jana Jumatano mjini Nairobi, Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia, Dakta Sorena Sattari amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono kikamilifu ushirikiano baina ya Nairobi na Tehran katika uga wa teknolojia.

Ameashiria mafanikio ya Iran katika uzalishaji wa vifaa na suhula za matibabu katika kipindi hiki cha janga la corona na kueleza kuwa, ili kuweza kukabiliana na virusi vya corona, kampuni za kitaalamu za Iran zimefanikiwa kuzalisha vifaa mbalimbali vya tiba kama mashine za hewa ya oksijeni zinazohitajika na waliokumbwa na ugonjwa wa Covid-19, vipimajoto vya kidijitali, mashine za kupiga picha mwili wa mwandamu za CT Scan n.k.

Sattari amebainisha kuwa, hatua zote hizi zimepigwa nchini Iran katika hali ambayo, licha ya kuonesha nia njema katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini inapitia kipindi kigumu cha vikwazo shadidi vya Marekani. 

Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia ameongeza kuwa, "katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia ustawi mkubwa katika nyuga za teknolojia na ubunifu katika nchi yetu. Nafasi ya Iran katika uzalishaji wa sayansi duniani imekwea kutoka 34 hadi 16, na ni ya kwanza katika eneo (la Asia Magharibi)."

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa Kenya, Joseph Mucheru na Rais wa Jumuiya ya Biashara ya Kenya ni mingoni mwa wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo wa Kituo cha Ubunifu na Teknolojia cha Iran (IHIT) katika mtaa wa Kilimani jijini Nairobi.

Wawakilishi wa mashirika 40 ya kiteknolojia ya Iran katika nyuga za petrokemikali, nishati jadidika, utengenezaji dawa, bioteknolojia na nanoteknolojia wameshiriki uzinduzi huo pia na kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji wa Kenya.