Mwakilishi wa Hamas nchini Iran: Utawala wa Kizayuni hauaminiki kwa ahadi yoyote
Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) nchini Iran amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni si wa kuaminiwa kwa ahadi yoyote lakini katika vita vya siku 12 utawala huo umelazimika kukubali masharti ya wanamapambano wa Palestina.
Khalid Qaddumi amesema kuwa, Benjamini Netanyahu naye ameshatupwa katika jalala la taka za historia na hata serikali mseto ya utawala huo ghasibu inalegalega. Qaddumi alibainisha haya jana katika hafla ya kuzindua kitabu kiitwacho "Golanl."
Mwakilishi wa Hamas hapa nchini ameongeza kuwa, hii ni moja ya ishara za ushindi wa muqawama pale shakhsia wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni wanapokimbilia kutoa vitisho na kutumia mabavu.
Qaddumi amesema, wakati huo huo, hali hii ya mambo imeandaa fursa ya kuhuishwa misaada ya kibinadamu na kuiunganisha tena Palestina. Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) hapa nchini Iran aidha amesema kuwa, harakati hiyo imeweza kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi za Kiislamu na kwamba Hamas imepanga kukutana na kufanya mazungumzo hapa nchini pia ili kuendeleza harakati za muqawama.
Khalid Qaddumi amesema kuwa, lengo la kufanyika mikutano hii ni kujadili suala muhimu la nafasi ya Umma wa Kiislamu na kwamba mikutano yote hii ni fursa nzuri kwa ajili ya kuanzisha umoja na kuwa na mshikamano madhubuti.
Kitabu kilichopewa jina la " Golan" ambacho kilizinduliwa jana hapa Tehran kimechapishwa kwa lugha ya Kiarabu; na kinatazamiwa kuchapishwa pia katika lugha za Kifarsi na nyinginezo.
Kitabu hicho kinaelezea umuhimu wa milima ya Golan ya Syria, na kimezinduliwa wakati huu wa kukaribia kumbukumbu ya kukaliwa kwa mabavu miinuko ya Golan ya Syria na utawala wa Kizayuni wa Israel.