Iran yaitaka dunia ikomeshe jinai za Israel dhidi ya Wapalestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kufanya jinai na uhalifu dhidi ya Wapalestina.
Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, taasisi na mashirika ya kimataifa yanapaswa kutekeleza wajibu wao wa kisheria na kiutu kwa Wapalestina, na kuchukua hatua za kukomesha sera za mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid za Israel.
Khatibzadeh amelaani vikali kitendo cha walowezi wa Kizayuni kuendeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Wapalestina wakazi wa kitongoji cha Sheikh Jarrah katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds katika siku za hivi karibuni wakisaidiwa ma jeshi la Israel.
Wiki iliyopita pia, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria ilitoa wito wa kukomeshwa hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuharibu nyumba za Wapalestina na kuwafukuza katika ardhi na makazi yao.
Taarifa ya wizara hiyo ilisema, amri ya maafisa wa utawala unaoikalia kwa mabavu Quds ya kuwafukuza Wapalestina katika kitongoji cha Sheikh Jarrah ni jinai ya kivita, kitendo cha kikatili na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu.
Katika siku za hivi karibuni, miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jodan likiwemo eneo la Sheikh Jarrah imekumbwa na mapigano baina ya wananchi wa Palestina kwa upande mmoja na wanajeshi na walowezi wa Kizayuni kwa upande wa pili.