Kuongezeka miamala ya kibiashara kati ya Iran na wanachama wa Jumuiya ya Shanghai
(last modified Tue, 03 May 2022 04:46:22 GMT )
May 03, 2022 04:46 UTC
  • Kuongezeka miamala ya kibiashara kati ya Iran na wanachama wa Jumuiya ya Shanghai

Ushirikiano wa Iran na nchi za ukanda huu ambao ni katika siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu hasa katika serikali ya hivi sasa, umezaa matunda mengi mazuri yakiwemo ya kuongezeka mabadilishano ya kibiashara baina ya Tehran na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Sayyid Ruhullah Latifi, Msemaji wa Idara ya Forodha ya Iran amesema, katika mwaka wa 1400 Hijria Shamsia, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kilifikia tani milioni 55 zenye thamani ya dola bilioni 37.2. Kiwango hicho kinaonesha kuweko ongezeko la asilimia 33 la uingizaji na usafirishaji nje bidhaa baina ya nchi hizo.

Sayyid Latifi ameongeza kuwa, kiwango cha bidhaa za Iran zilizotumwa kwa nchi 11 wanachama wa jumuiya hiyo pamoja na wanachama watazamaji ni kama ifuatavyo: Katika kipindi hicho, China imenunua bidhaa za Iran zenye thamani ya dola bilioni 14 na milioni 232 ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na miamala ya huko nyuma. Afghanistan ilinunua bidhaa za Iran zenye thamani ya dola bilioni moja na milioni 839 ikiwa kuna upungufu wa asilimia 20 ikilinganishwa na miamala ya huko nyuma. Amma India katika mwaka wa Kiirani wa 1400 Hijria Shamsia ilinunua bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu zenye thamani ya dola bilioni 1 na milioni 818 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 ikilinganishwa na miamala ya kabla ya hapo.

Muqama wa wananchi wa Iran na taufiki ya Allah imesambaratisha vikwazo vya madola ya kibeberu hasa Marekanidhidi ya Iran

 

Kuongezeka kwa kiwango kikubwa biashara za Iran  na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kunashuhudiwa chini ya kivuli cha kuzingatiwa zaidi masuala ya kiuchumi na kibiashara katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa. Hatua ya Tehran ya kuunda kitengo maalumu cha udiplomasia wa kiuchumi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilikuwa ni hatua muhimu iliyofanikisha jambo hilo hususan katika miamala ya kibiashara ya baina ya Jamhuri ya Kiislamu na majirani zake pamoja na nchi za Asia na Eurasia.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai ni chombo cha baina ya nchi mbalimbali na kazi yake kubwa na kuimarisha ushirikiano wa pande kadhaa wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa baina ya wanachama wake. Jumuiya hiyo iliundwa mwaka 1996. Wanachama wenye mchango mkubwa zaidi katika jumuiya hiyo ni nchi mbili za China na Russia. Mbali na wanachama wa asili, mwanzoni mwa mwaka 2004 Milaadia, Mongolia ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji ikifuatiwa na nchi za  Iran, Pakistan, India na Afghanistan mwaka mmoja baadaye yaani 2005. Baada ya hapo, Belarus nayo ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji wa jumuiya hiyo, ambayo hivi sasa wanachama wake ni China, Russia, Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzstan, Tajikistan, India na Pakistan. Mwezi Disemba 2021 Iran ilikubaliwa kuwa mwanachama kamili wa jumuiya hiyo. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutembelea mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

 

Faeze Moradi Haghighi, mtalamu wa masuala ya kiuchumi anasema: Tarehe 17 Septemba 2021 Iran ilipokewa kuwa mwanachama kamili ya Jumuiya ya Shanghai kwa kupigiwa kura za ndio na wanachama wote. Hivi sasa lakini uanachama wa Iran katika jumuiya hiyo si wa daraja ya kuweza kupiga kura. Kuna masharti kadhaa ya kuweza kufikia hatua hiyo kama ya wanachama waasisi wa jumuiya hiyo. Hali maalumu itakayokuwa nayo Iran katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili ijayo ndiyo itakayoamua kupewa haki Tehran ya kupiga kura kwenye jumuiya hiyo muhimu. 

Naye Bijan Tafzili, mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa anasema: Hatua ya Iran ya kukubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni ushindi mkubwa katika siasa na sera za kigeni za serikali ya Iran. Jambo hilo linaonesha kufeli na kushindwa njama za Marekani za kujaribu kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itengwe kimataifa. Ushindi huo imeupata Iran wakati huu ambapo ushirikiano baina ya Russia, China na nchi za Asia ya Kati unazidi kuwa mkubwa.

Tags