Iran: Kama US inapigania kweli haki za binadamu, iache kuwasaidia magaidi
Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imesema iwapo Marekani inataka kupambana kwa dhati na ugaidi, sharti iachane na tabia yake ya kuunga mkono makundi ya kigaidi kama lile la Kumalah.
Jarida la Kimarekani la News Week limeripoti kuwa, kiongozi wa kundi la kigaidi la Kumalah ameomba msaada na uungaji mkono wa Marekani, ili kuidhuru taifa la Iran.
Genge hilo la kigaidi la Kikurdi limeua mamia ya Wairani katika eneo la Mahabad, magharibi mwa Iran na katika maeneo mengine ya nchi.
Ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran katika UN imebainisha kuwa, kama Marekani inapigania kweli haki za binadamu, basi iache kuyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi kama Kumalah.
Hapo awali Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ilisisitiza kuwa, diplomasia haikuweza kukomesha kuwepo kwa magaidi kaskazini ya Iraq na ndio maana Iran imelazimika kutumia nguvu za kijeshi.
Mbali na Kumalah, makundi mengine ya kigaidi yenye makao kaskazini mwa Iraq na yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni ili kuzusha uasi na kuanza kujitenga baadhi ya maeneo ya nchi ni pamoja na Chama cha Kurdistan Democratic (KDP), na Chama cha Free Life of Kurdistan ambacho pia kinajulikana kama PJAK.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesisitiza kuwa, makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni yamekuwa yakipokea fedha kutoka nchi ajinabi ili yachochee ghasia nchini.
Ahmad Vahidi alisema hayo jana Alkhamisi akihutubia mkutano katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Utafiti cha Azadi, Bewa la Tehran na kuongeza kuwa, baadhi ya wafanya ghasia wamekuwa wakipokea pesa ndani ya kila dakika 15.
Ameashiria mfano mmoja, ambapo mtu mmoja amekuwa akipokea kwenye akaunti yake ya benki baina ya dola 750 na 900 katika kila dakika 10 hadi 15.