Oct 25, 2022 13:34 UTC
  • Taasisi na shakhsia kadhaa wa EU wataongezwa kwenye orodha ya vikwazo ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amedokeza kuwa karibuni hivi majina ya taasisi na shakhsia kadhaa wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya yataongezwa kwenye orodha ya vikwazo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanachuo wa Iran (ISNA), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ameashiria vikwazo zilivyowekewa taasisi saba na maafisa 13 wa Uingereza kutoka vituo vya televisheni vya "Iran International" na "BBC Farsi" kwa kosa la kuhamasisha mauaji, machafuko na misimamo ya kufurutu mpaka, ambavyo vilitangazwa na wizara ya mambo ya nje wiki iliyopita na akabainisha kuwa, "mnamo siku zijazo, majina ya taasisi kadhaa na shakhsia kutoka Umoja wa Ulaya yataongezwa pia kwenye orodha ya vikwazo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amir-Abdollahian ameyasema hayo atika kikao cha Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kilichofanyika kwa kuhudhuriwa na mkuu wake Hujjatul Islam Gholamhossein Mohseni Ajeei pamoja na wajumbe wa baraza hilo.

Tarehe 19 Oktoba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitangaza katika taarifa kuhusu vikwazo zilivyowekewa taasisi na shakhsia kadhaa wa Uingereza. Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia utoaji viza na kuingia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran watu waliowekewa vikwazo, kuzuiliwa mali na milki zao katika ardhi iliyo chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzuiwa akaunti zao za benki katika mfumo wa fedha na benki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../

 

Tags