Oct 03, 2023 06:40 UTC
  • Nasrullah: Lazima Wazayuni waisikie sauti ya Umma wa Kiislamu kuhusiana na kibla cha kwanza cha Waislamu

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, Umma wa Kiislamu unapaswa utekeleze wajibu wake kwa watu wa Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa, na akasisitiza kuwa: Wazayuni lazima waisikie sauti ya Umma wa Kiislamu kuhusiana na Kibla cha kwanza cha Waislamu.

Kwa mujibu wa mtandao wa al-Manar wa Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliyekuwa akihutubia kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume Muhammad SAW, amesema Umma wa Kiislamu unapaswa uwajibike kwa yale yanayowasibu watu wanaojitolea mhanga wa Palestina na Msikiti wa Al-Aqsa na akasisitiza kwamba, lazima Wazayuni waisikie sauti ya Ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na Kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.

Nasrullah amesema: "suna ya kuhuisha sikukuu za kidini ni sehemu ya utambulisho wa kuitamaduni na kifikra, na kama ilivyo Idul-Fitr na Idul-Adhhaa, kuna siku zingine kubwa na tukufu katika historia yetu ambazo zinawajumuisha pamoja Waislamu".

Katibu Mkuu wa Hizbullah amelaani shambulio la kigaidi la kuripuliwa misikiti ya Sunni nchini Pakistan na akasema: tunalaani kitendo cha kigaidi cha watenda jinai wa kitakfiri walioripua misikiti ya Sunni nchini Pakistan kwa kisingizio cha kuadhimishwa Maulidi ya Mtume SAW.

Sayyid Hassan Nasrullah amebainisha kuwa, wapo wanaotaka kuishusha hadhi ya mwanadamu hadi kiwango cha chini kabisa kwa kuendeleza ushoga na uhayawani na akaongeza kuwa: wanatumia vita vya vyombo vya habari au kile kinachoitwa vita laini kudhoofisha mataifa, lengo ambalo hawakuweza kulifikia kwa vita vya kijeshi.

Nasrullah amebainisha kuwa: nchi yoyote inayoelekea kwenye mkondo wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni inapasa ilaaniwe, kwa sababu maana ya hatua hiyo ni kuiacha mkono Palestina na kumuimarisha adui, na hivyo haipasi kuvumiliwa.../


 

 

Tags