Feb 29, 2024 03:02 UTC
  • Lolwah Al-Khater: Hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel Gazah ni mauaji ya kimbari

Lolwah Al-Khater, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar amesema kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gazah ni kielelezo cha wazi cha mauaji ya kimbari.

Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar, mbali na kukosoa kuendelea jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gazah ametoa mwito wa kusitishwa mara moja vita katika eneo hilo.

Amesema pia kuwa, tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gazah (Oktoba 7), Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa mara 3 kutoa azimio la kusitisha mapigano, na kwa mara ya 45 katika historia, limeshindwa kutoa azimio la  kusitisha vita.

Waziri huyo wa Qatar ameongeza kuwa, baadhi ya mataifa makubwa yanapaswa kuacha kuunga mkono utawala wa Kizayuni unaojiona kuwa nje ya sheria za kimataifa.

 

Wapalestina wasiopungua 29,000 wameuawa shahidi tangu Israel ianzishe mashambulio ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gazah

 

Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar, ameyataja mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gazah kuwa ni "mauaji ya kimbari ya watoto" na kusema: Vita vya Gazah vimefichua unafiki na sera za kindumakuwili za madola ya Magharibi kwa ulimwengu wote. Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar ameongeza kuwa: Jeshi la Israel limekiuka sheria zote za haki za binadamu za mikataba na hati za Umoja wa Mataifa.

Mwezi wa tano wa vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gazah unaelekea ukingoni. Vita hivi vimeandamana na mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gazah.

Tags