Mar 18, 2024 07:35 UTC
  • Makundi ya Palestina yako tayari kukabiliana na njama za pamoja za Marekani na utawala wa Kizayuni

Mustafa al-Barghouthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina ametahadharisha kuhusu njama mpya ya pamoja ya serikali ya Marekani na utawala haramu wa Israel kuhusu ujenzi wa bandari au gati la muda huko Gaza.

Al-Barghouthi imesema kuhusu kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kwamba, njia lazima zifunguliwe na kuwa iwapo Marekani itaamua, inaweza kuilazimisha Israel kufungua barabara za nchi kavu na kufikisha msaada kwa Wapalestina ndani ya masaa 24. Lakini badala ya kufanya hivyo, sasa inazungumzia ujenzi wa gati na bandari ambayo inaweza kuchukua miezi kadhaa kukamilika.

"Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina ameongeza kuwa: 'Inasemekana kwamba jukumu la kusimamia usalama wa bandari hiyo litapewa Israel, jambo ambalo lina maana kwamba Israel itaruhusiwa kuimarisha ukaliaji mabavu wake huko Gaza na hilo linahesabiwa kuwa jambo la kudumu na wala sio la muda." Amesema, hatua ya utawala haramu wa Israel kuruhusiwa kuharibu miundombinu yote huko Gaza inatoa uwezekano wa watu wa ukanda huo kufukuzwa kabisa na kwamba huenda bandari hiyo ikatumika kwa madhumuni hayo.

Mustafa a-Barghouthi

Mapema katika hotuba yake ya kila mwaka, Rais Joe Biden wa Marekani alisema kuwa nchi hiyo itatengeneza bandari ya muda karibu na Gaza ili kufikisha misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.

Biden ametoa matamshi hayo katika hali ambayo watu wa Gaza wamekabiliwa na mashambulizi makali ya jeshi la Kizayuni katika miezi ya hivi karibuni ambapo Wazayuni wameruhusiwa kuendelea kuua kwa umati watu wasio na ulinzi wa eneo hilo, hasa wanawake na watoto, na wakati huo huo kuharibu miundombinu kwa lengo la kuwalazimisha wahame ardhi na makazi yao ya asili. Suala jingine muhimu ni wakati wa kujengwa bandari hiyo ya muda ambapo kwa kutilia maanani kuwa vita vingali vinaendelea, ni wazi kuwa ujenzi wake utachukua miezi kadhaa kabla ya kukamilika. Muda mrefu wa ujenzi huo utaupa fursa inayofaa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Magharibi hasa Marekani, kuweza kuizingira zaidi Gaza.

Mbali na njia hizo zisizofaa na zinazochukua muda mrefu za Wamarekani, njia bora zaidi ya kuwasaidia watu waliozingirwa wa Gaza ni kuwafungulia njia za ardhini ambazo zinadhibitiwa na jeshi la Kizayuni. Makundi ya Wapalestina daima yamekuwa yakitoa wito wa kukomeshwa mzingiro huo na kufunguliwa njia za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Gaza. Umoja wa Mataifa pia umepitisha azimio la kutaka kusitishwa mzingiro huo, jambo ambalo linapingwa na Marekani.

Juliette Touma, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) anasema: "Tunakaribisha kikamilifu juhudi zozote za kupeleka misaada zaidi ya kibinadamu Gaza ili kuwasaidia watu wa eneo hili. Hata hivyo, kuna njia bora zaidi, nafuu na ya haraka zaidi ya kupeleka misaada Gaza, nayo ni kupitia nchi kavu. Takriban malori 500 ya misaada yanahitajika kila siku ili kukidhi mahitaji ya raia wa Palestina huko Gaza."

Juliette Touma

Watawala wa Marekani, kwa kuwasilisha mipango kama vile ya kujenga gati, ambayo kivitendo haitawezekana kutekelezeka, kwa hakika wanatekeleza matakwa ya mshirika wao mkuu, utawala wa Kizayuni, ambao unaendelea kuzuia na kupuuza maazimio yote ya Umoja wa Mataifa kuhusu Gaza. Hii ni katika hali ambayo suluhisho rahisi na la busara zaidi ni kufungua njia za nchi kavu ili misaada iweze kuwafikia watu wa Gaza kwa urahisi na haraka.

Baada ya kuanza operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, makundi ya muqawama ya Palestina yamethibitisha kuwa yanafahamu vyema matukio ya kisiasa na njama fiche za watawala wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni, na kuwa hayako tayari kusimamisha mchakato wa kuendeleza mapambano yao ambayo katika miezi ya hivi karibuni yamekuwa na matokeo chanya kwa taifa la Palestina.

Tags