Mar 29, 2024 11:59 UTC
  • HAMAS: Misimamo ya Israel imekwamisha mazungumzo ya Doha

Mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema mazungumzo ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza yamegonga mwamba huko Doha, mji mkuu wa Qatar kutokana na misimamo isiyoeleweka ya utawala haramu wa Israel.

Mohammad Nazzal, mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesema hayo leo Ijumaa katika mahojiano na televisheni ya al-Jazeera na kuongeza kuwa, "Hakujashuhudiwa maendeleo mazuri kwenye mazungumzo ya Doha licha ya jitihada za wapatanishi, kutokana na misimamo ya kuyumba ya utawala wa Kizayuni."

Mazungumzo hayo ya usitishaji vita Gaza na kubadilishana mateka kwa upatanishi wa Qatar na Misri yalikuwa yamejikita kwenye kufungua njia za kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Gaza na kubadilishana mateka.

Nazzal amebainisha kuwa, "Makubaliano ya kubadilishana mateka yanawezekana tu kwa kusitishwa kikamilifu uvamizi wa kijeshi dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza."

Harakati hiyo ya muqawama inasisitiza kuwa, mapendekezo ya kundi hilo la mapambano ya Kiislamu kwa ajili ya usitishaji vita Gaza yanaendana kikamilifu na uhalisia wa mambo kwa namna ambayo adui hawezi kuukataa. 

Mohammad Nazzal, mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS 

HAMAS inataka kusitishwa vita, kurejea wakimbizi, kutolewa misaada ya kibinadamu, kuanza ujenzi mpya wa Gaza, na kuondoka vikosi vya utawala ghasibu katika eneo la Gaza.

Mohammad Nazzal, mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ameeleza bayana kuwa: Vitisho vya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu vya kuuvamia na kuushambulia kijeshi kupitia ardhini mji wa Rafah ulioko kusini ya Ukanda wa Gaza haviwashtui wala kuwababaisha wanajihadi wa HAMAS. 

Tags