Feb 06, 2023 13:04 UTC
  • Colin Powell
    Colin Powell

Miaka 20 iliyopita yaani Februari 5, 2003, Colin Powell, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alishiriki katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuonyesha bomba la majaribio lililokuwa na mada za kimeta na kudai kuwa ni ushahidi wa kuwepo silaha za maangamizi ya umati nchini Iraq.

Jana tarehe 5 Februari ilikuwa siku ya kumbukumbu ya miaka 20 ya maafa ya uongo mkubwa zaidi ambao hadi sasa Marekani imeshindwa kuuthibitisha. Matokeo ya kikao hicho cha Baraza la Usalama ni uvamizi wa Marekani na washirika wake na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Iraq, kuondolewa madarakani utawala wa kisiasa wa nchi hiyo, mauaji ya mamia ya maelfu ya watu na wengine kufanywa vilema, mamilioni ya wakimbizi na kuibuka idadi kubwa ya makundi ya kigaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Hata hivyo silaha za maangamizi makubwa ambazo zilitajwa kuwa sababu ya mashambulio hayo na kwa hakika sababu ya uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq, hazikupatikana kamwe.

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 katika miji ya New York na Washington, utawala wa George W. Bush uliishambulia Afghanistan mwezi Oktoba 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na Machi 2003, uliishambulia Iraq kwa kisingizio cha kuharibu silaha za maangamizi ya halaiki. Uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iraq, ambao ulitekelezwa kwa amri ya George W. Bush, rais wa wakati huo wa Marekani, mbali na hasara kubwa za mauaji ya Wairaqi, vilevile ulisababisha vifo vya askari elfu kadhaa wa Marekani, kuitwisha nchi hiyo gharama kubwa za kiuchumi na kutia doa katika nafasi na hadhi yake kimataifa.

Uvamizi wa askari wa Marekani nchini Iraq 

George Bush alianzisha vita vya maangamizi ya binadamu dhidi ya Iraq huku Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na mashirika mengine ya ujasusi yakishuhudia kwamba, Ikulu ya White House iliudanganya umma ili kuhalalisha mashambulio yake huko Iraq, nchi ambayo haikuwa imeishambulia Marekani au hata kutoa vitisho vya kuishambulia. Baada ya uvamizi wa karibu miaka 9, kikundi cha mwisho cha wanajeshi wa Marekani kiliondoka Iraq Desemba 15, 2011. Vita vya Marekani nchini Iraq viliua zaidi ya Wairaqi laki moja na thalathini elfu. Katika vita hivyo pia, wanajeshi wasiopungua 5,000 wa muungano wa majeshi ya Magharibi wengi wao wakiwa Wamarekani, waliuawa. Zaidi ya wanajeshi 36,000 wa muungano huo walijeruhiwa, wengi wao wakiwa Wamarekani.

Wakati Bush alipoishambulia Iraq, alidai kuwa shambulio hilo lilianzishwa ili kuipokonya nchi hiyo silaha za maangamizi ya halaiki, kuwakomboa watu wake, na ili dunia isalimike na hatari kubwa. Bush alitangaza mwisho wa vita vya Iraq baada ya ushindi wa awali wa Marekani nchini humo na kuondolewa madarakani utawala wa Baath. Hata hivyo ukweli ni kwamba, vita vya Marekani nchini Iraq kivitendo vimekuwa vita vya msuguano wa miaka kadhaa, ambavyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu, na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Mbali na hasara za mauaji ya watu za vita vya Iraq, vita hivyo pia vilikuwa na gharama kubwa za kifedha, kama ilivyofichuliwa na ripoti nyingi zilizochapishwa na vituo vya wasomi vya Marekani. Kwa mfano tu kituo cha Kennedy katika Chuo Kikuu cha Harvard kilitangaza katika ripoti yake ya mwaka 2013 kwamba vita vya Iraq na Afghanistan ndivyo vita vyenye gharama kubwa zaidi katika historia ya Marekani, na kwa ujumla viligharimu kati ya dola trilioni nne hadi sita, ambayo ni sawa na dola 75,000 kwa kila familia ya Marekani. Gharama hizo zinajumuisha huduma za matibabu za muda mrefu na fidia kwa ulemavu wa kimwili wa askari, uboreshaji wa vifaa vya kijeshi na gharama za kijamii na kiuchumi. Gharama zingine nyingi za muda mrefu za vita hivyo zinahusiana na ulipaji wa deni la trilioni za dola. Mbali na hayo, gharama kubwa zinatumiwa kutayarisha silaha za kuchukua nafasi ya vifaa vya kijeshi vilivyotumika katika vita hivyo. Kwa ufupi tunaweza kusema kuwa, hali mbaya ya kifedha ya Serikali ya Federali ya Marekani, hasa katika suala la nakisi ya bajeti na deni la taifa, imesababishwa kwa kiasi kikubwa na sera za kivita za tawala za Bush na Barack Obama huko Iraq na Afghanistan.

Bush na Bleir walianzisha vita dhidi ya Iraq

Nukta muhimu ni kwamba maafa na masaibu haya kwa wananchi wa Iraq kimsingi yalihalalishwa kwa kutegemea uongo mkubwa, yaani madai ya kuwepo silaha za maangamizi ya umati nchini Iraq. Hii ni licha ya kwamba, ripoti za Umoja wa Mataifa zilionyesha kuharibiwa kwa silaha hizo. Kulingana na ripoti ya "Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kimkakati" mwaka 2002, maghala mengi ya silaha za kemikali na baolojia ya Iraq ambayo yaliorodheshwa na mkaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, Hans Blix, yalikuwa yameharibiwa kabla ya uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwezi Machi 2003. Baada ya kukaliwa kwa mabavu Iraq, ukaguzi wa kina uliofanywa na Umoja wa Mataifa haukupelekea kupatikana silaha za maangamizi ya umati katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita.

Robert Draper anaandika katika kitabu "To Start a War: How the Bush Administration Took America into Iraq" kwamba: "Iraq haikuwa na mpango wa nyuklia au gesi zenye sumu na roketi zenye virusi hatari. Jopo la Umoja wa Mataifa lilichunguza kwa miezi kadhaa lakini halikupata silaha haramu huko Iraq."

Tags