Kuongezwa muda wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria
Umoja wa Ulaya ukiendeleza siasa zake za chuki na uadui dhidi ya serikali halali ya Syria, umeongeza muda wa vikwazo vyake dhidi ya nchi hiyo.
Umoja wa Ulaya umesema katika taarifa yake ya siku ya Jjumatatu kwamba, muda wa vikwazo vya umoja huo dhidi ya Syria umeongezwa kwa mwaka mmoja mwingine yaani hadi Juni mwaka ujao.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imeeleza kuwa, vikwazo hivyo mbali na kuilenga serikali ya Syria vinazijumuisha pia serikali na tawala zinazounga mkono serikali ya Damascus. Kwa mujibu wa vikwazo hivyo kwa sasa shakhsia 240 na asasi 67 za Syria zinahusishwa na vikwazo vya safari na kuzuiwa mali zao.
Licha ya kulijitokeza baadhi ya matumaini kuhusiana na kuwepo mabadiliko katika misimamo ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na mgogoro wa Syria, lakini kuongezwa muda wa vikwazo vya asasi hiyo ya Ulaya dhidi ya serikali ya Damascus ni ishara kwamba, viongozi wa ngazi za juu wa EU wangali wanataka kuishinikiza serikali halali ya Rais Bashar al-Assad.
Nukta muhimu ni hii kwamba, muda wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria umeongezwa sambamba na kufanyika safari ya Rais Vladimir Putin wa Russia huko nchini Ufaransa na mazungumzo yake na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo jambo ambalo linaweza kuonyesha utendaji halisi wa umoja huo mkabala na mgogoro wa Syria.
Kwa hakika kuendelea vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria maana yake ni kuweko mtazamo hasi na usiofaa wa umoja huo katika njia ya kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu, mgogoro ambao uliibuka mwaka 2011 kwa himaya ya kila upande ya Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya na ya Kiarabu kwa makundi ya kigaidi katika nchi hiyo. Ufaransa na Uingereza zikiwa wanachama wawili wa Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2011 zikiwa na lengo la kusukuma mbele gurudumu la malengo jumla ya Muungano wa Kiarabu-Kimagharibi ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad, zimejikita katika kuyapatia makundi ya kigaidi misaada ya kila aina zikidhani kwamba, kwa kuyatumia magaidi hao zitaweza kuisambaratisha serikali ya Syria.
Lengo jumla zaidi la madola hayo kwa hatua yao ni kutoa pigo kwa mhimili mkuu wa muqawama katika Mashariki ya Kati yaani Syria na kwa kuanguka serikali ya Damascus, mnyororo wa muqawama udhoofike katika eneo hili na kwa muktadha huo Harakati ya Hizbullah ya Lebanon itengwe na kudhoofika. Aidha sambamba na kufanikiwa malengo ya kuuangushwa utawala wa Syria, madola hayo yaweze kutoa pigo kwa nafasi ya Iran katika eneo na hatimaye kupelekea itengwe. Hata hivyo waanzishaji wa vita hivyo hawajafanikiwa kufikia malengo yao huko Syria. Hivi sasa hali ya mambo nchini Syria ni kwa maslahi ya serikali ya Damascus na waitifaki wake. Hii ni katika hali ambayo, nafasi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri hasa baada ya kukombolewa mji wa Halab imedhoofika mno na hivi sasa serikali ya Syria ikishirikiana na waitifaki wake yaani Russia, Iran na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inakamilisha mwenendo wa ushindi katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
Katika kipindi hiki juhudi za viongozi wa Umoja wa Ulaya zimejikiti zaidi katika kuonyesha taswira hasi ya mfumo unaotawala nchini Syria na wakati huo huo kujaribu kubadilisha msimamo wa Russia kuhusiana na mgogoro wa Syria.