Je, kwa nini vita vya Gaza haviishi?
Licha ya kupita siku 46 tangu kuanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, lakini bado hakuna dalili zozote za kumalizika vita hivyo.
Katika kipindi cha siku 46 zilizopita, zaidi ya Wapalestina elfu 13 300 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, ambapo elfu 5, 600 ni watoto na elfu 3 500 ni wanawake. Zaidi ya watu elfu 30 wamejeruhiwa hadi sasa. Wanahabari 64 wameuawa shahidi kutokana na vita hivyo. Vituo vya matibabu huko Gaza vimeharibiwa au kufungwa kabisa kwa sababu ya ukosefu wa mafuta ya kuendeshea mitambo. Vituo vya afya na matibabu vya Gaza pia havifanyi kazi kutokana na kuharibiwa au kukosekana mafuta. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (FAO) limetangaza kuwa karibu watu milioni 2.2 huko Gaza wanahitaji msaada wa haraka wa chakula. Shakhsia na taasisi mbalimbali zimekiri mara kwa mara kwamba, vitendo vya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza ni jinai ya wazi ya mauaji ya kimbari. Swali muhimu linaloulizwa ni kuwa je, ni kwa nini vita havisimami?
Inaonekana kuwa kuna sababu mbili zinazosababisha kutosimamishwa vita vya Gaza.
Sababu ya kwanza ni kwamba baada ya siku 46 za vita, utawala unaoikalia kwa mabavu Quds bado haujafikia malengo iliyokusudia. Kuachiliwa huru mateka na kuangamizwa Hamas yamekuwa malengo makuu mawili ya utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Gaza. Utawala wa Kizayuni haujafanikiwa kumwachia huru hata mateka mmoja jati ya mateka wake waliokamatwa na Hamas na wala haujui walikofichwa. Utawala huo uliadhani kuwa mateka hao walikuwa wamefichwa chini ya hospitali na shule, lakini imethibitika kuwa madai hayo yalikuwa ni uwongo mtupu wa Wazayuni na suala hilo limepelekea utawala huo kushindwa kijasusi. Ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu zinashuhudia maandamano dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu, na sababu kuu ya maandamano hayo ni kushindwa baraza hilo kurudisha nyumbani mateka wake. Aidha utawala huo si tu haujaweza kulitokomeza kundi la Hamas, bali wapiganaji wa Hamas wametoa pigo kubwa kwa utawala huo katika vita vya Gaza. Kusimamishwa vita katika hali hiyo kutachukuliwa kuwa ni kushindwa utawala wa Kizayuni na ushindi kwa wanamuqawama wa Palestina. Kuhusiana na hilo, John Kirby, Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani amesema: Bado hatuamini kwamba wakati mwafaka umefika wa kusimamishwa vita. Kusitishwa mapigano kuna maana ya kusimamishwa vita katika eneo lote la Gaza, ambapo kwa sasa jambo hilo litakuwa kwa manufaa ya Hamas.
Sababu ya pili ni kwamba nchi za Magharibi bado hazijachukua uamuzi wa kusimamisha vita. Wakati ambapo vita vya upande mmoja vinashindwa kupata ushindi na kupindukia mipaka, mashinikizo ya nje yanaweza kuandaa uwanja mzuri wa kupatikana suluhisho katika uwanja huo. Madola ya Magharibi kama walivyo Wazayuni yanafuatilia ushindi wa utawala ghasibu katika vita, jambo ambalo halionekani kufanikiwa hadi sasa. Yaakov Amidror, mshauri wa usalama wa taifa wa Israel kuanzia mwaka 2011 hadi 2013 na ambaye pia ni Jenerali mstaafu wa ngazi ya juu wa jeshi la Israel, anaamini kuwa serikali ya Tel Aviv hadi sasa haihisi mashinikizo halisi kutoka kwa Marekani. Anasema mashinikizo pekee kutoka kwa Washington ni kupunguzwa idadi ya raia wanaouawa na kuruhusu kuingia misaada zaidi ya kibinadamu huko Ukanda wa Gaza.