Israel yashambulia kwa mabomu shule 2 Gaza, 50 wauawa shahidi
Vikosi vya utawala haramu wa Israel vimeshambulia kwa mabomu shule mbili katika Ukanda wa Gaza na kuua shahidi makumi ya Wapalestina.
Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu zaidi ya 50 wameuawa shahidi katika hujuma hizo za anga zilizofanywa na ndege za kivita za Wazayuni katika eneo la al-Daraj, kaskazini mwa Gaza.
Aidha makumi ya watu wamejeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya kinyama ya Israel dhidi ya shule mbili ambazo zinatumika kama kambi za wakimbizi wa Gaza.
Mwezi uliopita pia, jeshi la Israel lilishambulia kwa mabomu Shule ya Al-Fakhoura na Shule ya Tal Al-Zaatar na kuua na kuwajeruhi zaidi ya Wapalestina 200 waliokuwa wamejihifadhi humo kutokana na uvamizi unaoendelea wa utawala huo wa Kizayuni huko Gaza.
Hivi karibuni, Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (ISESCO) lilitoa tamko kali likilaani mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya shule mbili kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuyataja kuwa ni "fedheha kwa ubinadamu" na "uhalifu wa kutisha".
Wakati huo huo, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamevamia mji wa Sa'ir, kaskazini mashariki mwa mji wa Khalil (Hebron) katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuua shahidi vijana watano wa Kipalestina; siku moja baada ya kuua vijana wengine wawili katika mji wa Qalqilyah, kaskazini magharibi wa eneo hilo.
Aidha Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza habari ya kijana mmoja wa Kipalestina kuuawa shahidi kwa kupigwa risasi na Wazayuni katika mji wa Qalandiya, kaskazini mwa mji wa Quds tukufu unaokaliwa kwa mabavu.
Wizara hiyo imesema idadi ya Wapalaestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi mwaka huu imefikia 465, wakiwemo 275 waliouawa shahidi tokea Oktoba 7 hadi sasa.
Vita vya maangamizi ya umati vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza vilivyoanza tangu Oktoba 7, hadi sasa vimesababisha vifo vya Wapalestina karibu 16,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.