Hamas yakanusha uongo wa Netanyahu, yasema kamwe haitaweka chini silaha
Afisa wa ngazi za juu wa harakati ya Hamas amekadhibisha uongo wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu eti kujisalimisha kwa wapiganaji wa harakati hiyo kwa jeshi la Israel akisema uongo huo ni kielelezo cha kufilisika na kushindwa utawala wa Kizayuni kutokana na mapambano makali ya wapigania uhuru wa Palestina.
Ghazi Hamad amesema hayo akikanusha uongo wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni aliyedai kwamba makumi ya wanachama wa Hamas walijisalimisha kwa jeshi la Israel katika siku chache zilizopita na kusema: Hamas kamwe haitakabidhi silaha zake, na wanamapambano hawatajisalimisha, bali watadumisha muqawama.
Hamad ameongeza kuwa: Matamshi yaliyotolewa na Netanyahu na makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni yanaonyesha kuwa licha ya kuwepo tofauti kubwa katika uwezo wa kijeshi wa pande mbili hizo, lakini Wazayuni wako katika mgogoro wa kisaikolojia unaosababishwa na vipigo vya muqawama.
Hamad pia amejibu kauli za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, ambaye ameitaka harakati ya Hamas kusalimu amri na kusema: Unapaswa kuwataka wavamizi wa ardhi ya Palestina wajisalimishe, na sio Hamas!
Afisa huyo wa Hamas amebainisha kuwa, yanayojiri katika medani ya vita ni kielelezo cha wazi kuwa utawala ghasibu wa Israel umeingia kwenye kinamasi ambacho hauwezi kutoka, na serikali ya Marekani pia ni mshirika wa jinai za Israel za kuua raia, kwa sababu inaendelea kuwapa silaha Wazayuni makatili.