Asilimia 61 ya nyumba za raia Ukanda wa Gaza zimebomolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105880-asilimia_61_ya_nyumba_za_raia_ukanda_wa_gaza_zimebomolewa
Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imeripoti kwamba asilimia 61 ya nyumba za raia wa Kipalestina huko Ukanda wa Gaza zimebomolewa katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 11, 2023 23:24 UTC
  • Asilimia 61 ya nyumba za raia Ukanda wa Gaza zimebomolewa

Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imeripoti kwamba asilimia 61 ya nyumba za raia wa Kipalestina huko Ukanda wa Gaza zimebomolewa katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imesema katika taarifa yake kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel hadi sasa limebomoa asilimia 61 ya makazi ya raia wa Palestina katika ukanda huo. Aidha imeelezwa kuwa maghasibu wa Kizayuni wamebomoa nyumba za raia zaidi ya 305,000 katika mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza. 

Taarifa ya Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imeongeza kuwa utawala wa Kizayuni umefanya uharibifu huo katika fremu ya maangamizi ya kizazi ya wananchi madhulumu wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.

Imesema, taasisi za kimataifa zinapasa kutilia maanani suala la kutokea maafa ya binadamu huko Ukanda wa Gaza; kwa sababu kila siku tunashuhudia nyumba nyingi za raia zikibomolewa na kuharibiwa katika eneo hilo. Maghasibu Wazayuni wametumia zaidi ya tani 52,000 za mada za milipuko katika mashambulizi ya kikatili dhidi ya Wapalestina, hospitali, shule na taasisi za kiraia huko Gaza.

Taarifa ya Idara ya Serikali ya Gaza imeeleza kuwa: Wakimbizi milioni moja na nusu wa Kipalestina wanaishi ndani ya Ukanda wa Gaza katika hali ngumu. "Tunashuhudia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza wakati huu wa kuwadia majira ya baridi. Kitendo cha kuzuia bidhaa za chakula na mahitaji mengine muhimu kuingia Ukanda wa Gaza kuna maana ya kutoa hukumu ya kifo kwa raia milioni mbli na laki mbili wa eneo hilo. 

Wakati huo huo msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesisitiza kuwa: Kuuliwa watoto  wa Kipalestina karibu 7,800 huko Gaza ni doa jeusi kwenye paji la uso wa ubinadamu.