Hizbullah: Tutaendelea kuishambulia Israel hadi ikomeshe jinai zake Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105952-hizbullah_tutaendelea_kuishambulia_israel_hadi_ikomeshe_jinai_zake_gaza
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kundi hilo la muqawama wa Kiislamu litaendelea kufanya mashambulizi ya ulipizaji kisasi dhidi ya Israel, madhali utawala huo wa Kizayuni unaendelea kumwaga damu za Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-12-13T07:46:34+00:00 )
Dec 13, 2023 07:46 UTC
  • Hizbullah: Tutaendelea kuishambulia Israel hadi ikomeshe jinai zake Gaza

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kundi hilo la muqawama wa Kiislamu litaendelea kufanya mashambulizi ya ulipizaji kisasi dhidi ya Israel, madhali utawala huo wa Kizayuni unaendelea kumwaga damu za Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono na kuwapa himaya wananchi madhulumu wa Palestina.

"Hizbullah itaendelea kushambulia maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel katika mpaka wa Lebanon, maadamu vita vya Wazayuni dhidi ya Gaza vinaendelea," Sheikh Qassim amenukuliwa akisema hayo na tovuti ya habari la al-Ahed ya Lebanon.

Mashambulio ya Hizbullah katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yameongezeka na kuwa makali zaidi baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Gaza, kufuatia kumalizika muda wa usitishaji vita wa muda.

Televisheni ya Bloomberg ya Marekani imefichua kuwa, mashambulio ya Hizbullah ya Lebanon huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, limekuwa jinamizi kwa walowezi wa Kizayuni wanaoishi kwenye maeneo hayo.

Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa: Inachokifanya Hizbullah ni mapambano halali na kujihami, na vile vile inatekeleza jukumu la kidini, kwa kuwa maadui wanaelewa tu lugha ya mabavu.

Kiongozi huyo mwandamizi wa kidini wa Lebanon ameongeza kuwa, kundi hilo la muqawama wa Kiislamu litaendelea kufanya mashambulizi ya ulipizaji kisasi dhidi ya Israel, kwa lengo la kuuzuia utawala huo haramu kufikia malengo yake hivi sasa na hata baadaye.