Onyo la Macron kuhusu kuharibiwa Gaza na Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106264-onyo_la_macron_kuhusu_kuharibiwa_gaza_na_wazayuni
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuangamizwa Ukanda wa Gaza kwa mashambulizi kipofu ya utawala haramu wa Israel huku mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yakiendelezwa na utawala huo katili katika ukanda huo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 21, 2023 22:59 UTC
  • Onyo la Macron kuhusu kuharibiwa Gaza na Wazayuni

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuangamizwa Ukanda wa Gaza kwa mashambulizi kipofu ya utawala haramu wa Israel huku mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yakiendelezwa na utawala huo katili katika ukanda huo.

Huku akiashiria kwamba hatupasi kuwa na dhana kwamba kupambana na ugaidi kuna maana ya kuangamizwa Gaza kwa mashambulizi kipofu na mauaji ya halaiki dhidi ya raia, Rais wa Ufaransa ameutaka utawala wa Kizayuni kusitisha mara moja mauaji ya aina hiyo kwa sababu hatua hiyo haifai na maisha ya watu wote ni sawa na yanathaminiwa. Rais Macron vilevile ametaka kulindwa maisha ya raia na kutekelezwa usitishaji vita wa kibinadamu huko Gaza.

Kauli hiyo ya Rais wa Ufaransa inatolewa katika hali ambayo yeye mwenyewe na waitifaki wake wengine wa Ulaya yalipoanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakaazi wa Gaza, walivitaja vita hivyo kuwa ni vita dhidi ya ugaidi na kuunga mkono jinai za Israel dhidi wananchi wasiokuwa na hatia wa Gaza.

Tangu vilipoanza vita vya Gaza, Ufaransa na Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya zimekuwa zikiunga mkono jinai za utawala huo na kuuawa Wapalestina kwa kuupatia utawala huo misaada ya kifedha na silaha.

Kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina Gaza

Watawala wa Ulaya wamekuwa wakiyataja maangamizi ya halaiki yanayofanywa na utawala katili wa Israek dhidi ya Wapalestina kuwa ni katika hatua ya kujilinda Israel na vilevile kupambana na ugaidi na hata wamekuwa wakipiga maandamano yanayofanywa na makundi ya kijamii ya kulaani mauaji ya Wapalestina kama vile kushambuliwa mahospitali, vituo vya kidini na kihistoria katika nchi hizo.

Pamoja na hali hiyo na kushtadi mauaji ya Wapalestina na mashambulizi ya kila upande ya Israel dhidi ya Gaza hivi sasa  viongozi wa Ulaya wamelazimika kuwalaumu kwa maneno matupu Wazayuni kutokana na mashinikizo ya weliowengi barani humo.

Hata kama idadi ya juu ya vifo na uharibifu mkubwa wa miundombinu na makazi ya raia unaofanywa na Israel dhidi ya taofa la Palestina hauwezi tena kutetewa na kuungwa mkono na waitifaki wa Magharibi wa utawala huo, lakini sasa viongozi wa Magharibi na hasa rais wa Ufaransa, wanatoa maneo matupu tu ya kutaka usitishaji vita utekelezwe na kusimamishwa mauaji ya wananchi wa Palestina lakini kwa hakika bado wanauunga mkono utawala huo.

Inaonekana kuwa msimamo wa Macron unalenga zaidi kuvutia hisia za wananchi wa nchi hiyo na nchi nyingine za Ulaya kuliko kuegemea kwenye nia halisi ya kusimamishwa mashambulizi dhidi ya Gaza.

Robert Fico, Waziri Mkuu wa Slovakia, amekosoa mtazamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu mzozo wa Gaza na kusema: Vifo vya watu 20,000 huko Gaza haviwezi kupuuzwa kwa sababu tu ya madai ya kujilinda Israeli. Ninawasisitizia viongozi wa Ulaya kuwa umoja huo umepoteza itibari na satwa yake kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kuchukua msimamo thabiti na wa pamoja juu ya kadhia ya Palestina.

Ofisi ya Habari ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetangaza katika ripoti yake kwamba idadi ya mashahidi huko Gaza tokea vilipoanza vita tarehe 7 Oktoba imefikia 20,000, ambapo 8,000 kati yao ni watoto na 6,200 ni wanawake.

Emmanuel Macron

Kwa mujibu wa ripoti hiyo majeruhi wa vita hivyo wamefikia elfu 52 na 600.

Huku hali ya kibinadamu katika ukanda huo ikizidi kuwa mbaya, Amnesty International katika taarifa yake imezitaka nchi za Ulaya kusimamisha jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na kutangaza usitishaji vita wa kudumu katika ukanda huo. Lakini kivitendo hakuna hatua muhimu zinazochukuliwa na Wamagharibi kukomesha jinai za Israel, na sasa inaonekana kuwa Emmanuel Macron amelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na kutaka kusitishwa vita hivyo kwa maneno matupu tu ili kujipatia itibari ya kisiasa.