Vita vya Gaza vyazuia wanafunzi elfu 600 wa Kipalestina kupata elimu
Mamlaka ya Palestina imetangaza kwamba kuendelea mapigano huko Gaza, kutazuia zaidi ya wanafunzi 600,000 wa Kipalestina kupata elimu.
Uharibifu mkubwa wa Gaza kutokana na mashambulizi ya kinyama ya jeshi katili la Kizayuni umekuwa na madhara makubwa kwa Wapalestina wanaoishi katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, shule 352 ambazo ni sawa na asilimia 70 ya shule za Gaza zimeharibiwa vibaya katika mashambulizi ya jeshi vamizi la Israel.
Wanajeshi hao pia wa utawala haramu wa Kizayuni wamezishambulia shule za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan karibu na ukuta wa kibaguzi na kuziba njia za mawasiliano.
Hadi sasa Wapalestina 22,000 wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, zaidi ya asilimia 70 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa kanali ya habari ya Al Jazeera, Sadiq al-Khadur, Msemaji wa Wizara ya Elimu ya Gaza ametangaza kuwa wanafunzi 625,000 wa Gaza wamekosa fursa ya kuendelea na masomo tokea ulipoanza uvamizi wa jeshi la Kizayuni katika ukanda huo tarehe 7 Oktoba.
Msemaji huyo amesema kiwango hicho ni cha wanafunzi wote waliokuwa wakisoma kabla ya vita.
Akirejelea idadi ya wanafunzi waliouawa shahidi, Sadiq Al-Khadur ameongeza kuwa takriban wanafunzi 4,000 wameuawa shahidi na wengine 7,000 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga na nchi kavu ya adui Mzayuni huko Gaza.
Msemaji huyo wa Wizara ya Elimu ya Gaza ameongeza kwamba zaidi ya walimu na wafanyakazi 210 wa idara ya elimu wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi hayo ya Israel.