Tangu Oktoba 17 vituo vya kijeshi vya Marekani Asia Magharibi vimeshambuliwa mara 115
(last modified Sat, 06 Jan 2024 03:47:17 GMT )
Jan 06, 2024 03:47 UTC
  • Tangu Oktoba 17 vituo vya kijeshi vya Marekani Asia Magharibi vimeshambuliwa mara 115

Afisa mmoja wa Marekani amekiri kuwa katika muda wa siku 81 zilizopita, ngome na vituo vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika eneo la Asia Magharibi vimeshambuliwa mara 115.

Gazeti la Washington Post limeashiria shambulio la kigaidi lililofanywa siku ya Alkhamisi mjini Baghdad na ndege zisizo na rubani za Marekani lililopelekea kuuawa shahidi watu watatu akiwemo Mushtaq Talib al-Saeidi anayejulikana kwa lakabu ya Al-Hajj Abu Taqawi, kamanda wa Brigedi ya 12 ya Al-Hashd al-Shaabi na mkuu wa operesheni za Harakati ya Nujabaa, na kuandika kuwa: katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni Marekani imeshambulia maeneo ya makundi mbalimbali nchini Iraq na Syria, mauaji ya Mushtaq Talib al-Saeidi yameongeza hatari ya kuzuka mvutano katika eneo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, uungaji mkono wa Marekani kwa Israel katika vita dhidi ya Gaza, pamoja na ongezeko la vifo vya raia wa Palestina, vimetoa motisha mpya kwa makundi ya ndani ya Iraq na Syria ya kufanya juhudi zaidi za kuyatimua majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani.
Afisa mmoja wa Marekani amesema bila kutaja jina lake kwamba, mashambulizi 115 yamefanywa kulenga vituo vya jeshi la nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi tangu Oktoba 17 (siku 81) na kueleza kuwa mashambulizi mengi yamefanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani au makombora au yote mawili.
Askari wa jeshi vamizi la Marekani wakiranda kwenye mitaa ya Iraq

Kwa mujibu wa afisa huyo, wanajeshi 2,500 wa Marekani wapo nchini Iraq kwa kisingizio cha kutoa "mafunzo na ushauri". Wanajeshi wengine wapatao 900 wa Marekani wamewekwa katika maeneo tofauti nchini Syria.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Muqawama wa Iraq hadi sasa umeshambulia kwa makombora na droni vituo vya kijeshi vya Marekani vya Ain al-Asad karibu na uwanja wa ndege wa Erbil, Harir Iraq na Kharab Al-Jir, Al-Shadadi, Al-Tanf, Al-Rimilan, Al-Maalikiyya, kambi za kijeshi zilizoko karibu na visima vya mafuta vya Konico na al Omar na kitongoji cha Sabz nchini Syria.
Lengo la operesheni za makundi ya muqawama dhidi ya ngome na vituo vya kijeshi vya Marekani limetangazwa kuwa ni kutoa mashinikizo kwa Ikulu ya White House ikomeshe uungaji mkono wake usio na kikomo kwa jinai za umwagaji damu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita dhidi ya Gaza.../

 

Tags