Azma thabiti ya serikali ya Iraq kuondolewa nchini humo wanajeshi wa Marekani
(last modified Sun, 07 Jan 2024 08:17:09 GMT )
Jan 07, 2024 08:17 UTC
  • Azma thabiti ya serikali ya Iraq kuondolewa nchini humo wanajeshi wa Marekani

Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza katika msimamo nadra kabisa juu ya ulazima wa kuondoka nchini humo wanajeshi vamizi wa Marekani.

Mohammed Shia' Al Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq ametangaza kuandaa ratiba na jedwali la kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq. Waziri Mkuu na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Iraq amesema hayo katika kumbukuumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa shahidi makamanda wa muqawama Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al-Mohandes  ambapo sambamba na kusisitiza kuwa, serikali ya Baghdad inapanga tarehe ya kuanza kazi ya kamati ya nchi mbili katika fremu ya hatua za mwisho zinazohusiana na mwisho wa uwepo wa jeshi la Marekani nchini Iraq.

Kadhalika al-Sudani amelitaja shambulio la wanajeshi wa Marekani dhidi ya makao makuu ya Harakati ya Kujitolea ya Wananchi ya al-Hashd al-Sha'abi kuwa ni la kigaidi ambalo limekiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. Msimamo huu wa Waziri Mkuu wa Iraq ni nadra sana katika miaka michache ya hivi karibuni na unahhesabiwa kuwa ni wa aina yake. Kauli za Al-Sudani na uwazi wake katika kukariri udharura wa kuondoka Iraq askari vamizi wa Marekani ni ithbati tosha ya kutoridhika kwa mamlaka ya Iraq na suala la kuendelea kuwepo kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mohammed Shia' Al Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq

 

Karim Al-Mohammadawi, mjumbe wa Kamisheni  ya Mahusiano ya Kigeni ya Bunge la Iraq, pia alitoa mwito wa kutumiwa nguvu na maandamano ya umma kuwafukuza wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq.

Katika miaka ya nyuma, wananchi wa Iraq pamoja na makundi na vyama mbalimbali vya siasa vimekuwa vikipaza sauti na kusisitiza takwa la kuondoka nchini humo wanajeshi wa Marekani

Wanajeshi wa Marekani wanaendelea kuwepo nchini Iraq katika hali ambayo hatua hiyo ni kinyume kabisa na mazungumzo na makubaliano ya hapo awali kati ya serikali za Baghdad na Washington. Kimsingi Marekani imekuwa ikikwepa kutekeleza jukumu lake kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.

Licha ya kufanyika duru kadhaa za mazungumzo ya kimkakati kati ya Baghdad na Washington kwa minajili ya kuhitimisha uwepo wa jeshi la Marekani huko Iraq kutokana na kumalizika kwa vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na kupasishwa na Bunge la Iraq mpango wa kuwafukuza wanajeshi wote wa kigeni katika ardhi ya nchi hiyo, lakini bado Marekani inakiuka azimio hili katika ardhi ya Iraq.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

 

Wanasiasa wa Iraq wanaamini kuwa, matokeo ya kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ni vifo na kujeruhiwa maelfu ya watu na kuharibiwa miundombinu ya kiuchumi ya nchi hiyo. Tathmini ya Benki ya Dunia pia inaonyesha kwamba uharibifu wa kiuchumi wa uvamizi wa kijeshi na kuendelea kuwepo kwa askari wa Marekani nchini Iraq umesababishha hasara ya zaidi ya dola bilioni 350 kwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Ijapokuwa takwimu rasmi na sahihi za idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la Marekani nchini Iraq bado hazijatolewa na kutangazwa bayana, lakini viongozi wa Iraq wamekuwa wakibainisha kuwa, kukaliwa kwa mabavu Iraq kumesababisha maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Licha ya kuenea malalamiko makubwa ya vyama mbalimbali, serikali na wananchi wa Iraq, lakini serikali ya Marekani haijatekeleza wajibu wake wa kuwaondoa kikamilifu wanajeshi wake katika ardhi ya Iraq.

Msimamo mpya wa Waziri Mkuu na viongozi wa Iraq unaonyesha azma yao thabiti na imara na juhudi kubwa za kutaka kuondolewa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq. Mamlaka za Iraq zinaamini kuwa, zina uwezo wa kukabiliana na makundi ya kigaidi na kudhamini usalama wa nchi yao, na kwa muktadha huo, hakuna tena haja ya kuendelea kuwepo nchini humo askari wa kigeni.

Tags