Yemen: Oparesheni dhidi ya utawala wa Kizayuni zinaendelea
Mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza kuwa jeshi la nchi hiyo litaendelea kutekeleza oparesheni dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Bahari ya Sham na katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo (Israel).
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa Ali al Qahum amesema: Oparesheni za jeshi la Israel katika ardhi za Palestina zinaendelea na kwamba oparesheni za Yemen katika Bahari ya Sham pia zitaendelea licha ya vitisho na hatua za uhasama za Marekani, Uingereza na Israel.
Al Qahum pia ametoa mkono wa taazia na pole kwa kuuliwa shahidi Saleh al Arouri Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kusisitiza kuwa: Yemen itaendelea na misimamo yake ya kuunga mkono muqawama wa Wapalestina kwa sababu Palestina ndio dira ya taifa hilo. Kiongozi huyo wa Yemen ameendelea kusema: Wamarekani wanapasa kuelewa kwamba si katika Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu) au popote pengine duniani wataweza kuilinda Israel."
Wakati huo huo Muhammad Ali al Houthi Mwakilishi wa baraza Kuu la Kisiasa la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amezitaka meli zinazopita katika Lango Bahari la Bab al-Mandab kutangaza kuwa hazina uhusiano wowote na utawala wa Israel.