Jan 12, 2024 03:55 UTC
  • US, UK zashambulia vituo vya Ansarullah Yemen kwa sababu ya msimamo wake wa kuwahami Wapalestina

Marekani na Uingereza zimeshambulia vituo kadhaa vya harakati ya Ansarullah kukabiliana na hatua ya harakati hiyo ya wananchi wa Yemen ya kuzishambulia meli zenye uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, kwa sababu ya vita vya mauaji ya kimbari na ya halaiki unavyoendesha utawala huo dhalimu dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo, vikisema yalihusisha ndege za kivita na makombora ya Tomahawk.
 
Harakati ya Ansarullah imesema mashambulizi hayo yalilenga mji mkuu Sana'a pamoja na miji ya magharibi ya al-Hudaydah, Sa'ada, na Dhamar na kulaani kile ilichokiita "uchokozi wa Marekani na ushiriki wa Uingereza."
 
Rais wa Marekani Joe Biden amethibitisha kufanyika mashambulio hayo, akisema yamefanywa na Marekani na Uingereza na kwa msaada kutoka Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi.
 
Biden amedai kuwa "hatasita" kuelekeza hatua zaidi dhidi ya maeneo ya Yemen.
 
Katika miezi ya hivi karibuni, harakati ya Ansarullah na Wanajeshi wa Yemen wamekuwa wakifanya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya meli zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel au zile zinazoelekea katika bandari za utawala huo wa kibaguzi kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza wanaoandamwa na vita vya kinyama vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.
Sayyid Abdul-Malik al-Houthi

Tangu vilipoanza tarehe 7 Oktoba, vita hivyo vimewaua shahidi Wapalestina wapatao 23,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 59,167. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamefia chini ya vifusi.

Hayo yanajiri wakati jana Alkhamisi Kiongozi wa harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen, Sayyid Abdul-Malik al-Houthi, alionya kuhusu jibu "kubwa" itakalotoa harakati hiyo kwa Marekani na washirika wake ikiwa wataendelea na mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi yake.

"Shambulio lolote la Marekani halitaachwa bila ya jibu. Mjibizo utakuwa mkubwa zaidi kuliko shambulio lililofanywa na ndege zisizo na rubani ishirini na idadi ya makombora kadhaa," ameonya kiongozi huyo.

Harakati ya Ansarullah ilishaeleza bayana kwamba ukiondoa meli zinazoelekea bandari za utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel, meli nyingine zote zitakuwa salama na hazitaandamwa na mashambulizi ya Yemen maadamu nchi zao hazimo au hazijapanga kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya Yemen.../

Tags