Jan 26, 2024 07:57 UTC
  • Tangazo la Marekani la kuwa tayari kwa mazungumzo ya kuhitimisha kuwepo kwake kijeshi nchini Iraq

Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, katika barua ambayo balozi wa Marekani mjini Baghdad, Alina Romanovsky aliiwasilisha siku ya Jumatano kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hossein, Washington imetangaza kuwa iko tayari kuanza mazungumzo na Baghdad ya kuhitimisha uwepo kijeshi wa nchi hiyo na washirika wake katika ardhi ya Iraq.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hossein (kulia) na Balozi wa US nchini Iraq Alina Romanovsky

Wakati malalamiko na upinzani dhidi ya kuendelea kuwepo askari 2,500 wa Marekani waliopiga kambi nchini Iraq yakiwa yamezidi kuongezeka, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ametangaza kuwa barua ya balozi wa Marekani mjini Baghdad itashughulikiwa na Waziri Mkuu Mohammad Shia al-Sudani na maafisa husika. Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema pia kuwa, suala hilo si geni, na tokea huko nyuma yameshawahi kufanyika mazungumzo ya kujadili kadhia hiyo kati ya maafisa wa nchi mbili za Iraq na Marekani na akaongeza kuwa, kuanza kwa mazungumzo hayo kulishajadiliwa tangu miezi kadhaa nyuma. Afisa huyo wa Washington ameendelea kueleza kwamba, katika kipindi chote cha kufanyika mazungumzo hayo, Marekani itaendelea pia kulinda haki yake kamili ya kujihami kijeshi.

 

Pamoja na hayo, nukta ya kutatanisha hapa ni kwamba siku kadhaa nyuma, yaani tarehe 16 Januari, wakati vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Iraq na Syria viliposhambuliwa, Washington ilitangaza kwamba, inakusudia kutuma wanajeshi wengine wapya 1,500 huko Iraq na Syria kutoka kikosi chake cha gadi ya taifa cha New Jersey kwa ajili ya kile ilichokiita, kupambana na kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).

Viongozi wa Iraq wameshatoa matamko mara kadhaa ya kutaka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo. Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu Mohammad Shia Al-Sudani, ambaye mapema Januari 2024, alisisitiza kwa mara nyingine tena wanajeshi wa Marekani waondoke haraka katika ardhi ya Iraq.

Baada ya mauaji ya kikatili ya Shahidi Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na Shahidi Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu wa Kikosi cha Al-Hashdu-Shaabi pamoja na waliofuatana nao yaliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad mnamo Januari 3, 2020, siku mbili baadaye, yaani tarehe 5 Januari bunge la Iraq lilipiga kura kutaka vikosi vya muungano wa kupambana na DAESH vikiwemo vya Marekani viondoke katika ardhi ya nchi hiyo.

Hata hivyo Washington iliendeleza msimamo unaopingana na sheria kwa kushikilia wanajeshi wake waendelee kuwepo nchini Iraq. Hatimaye, kutokana na mashinikizo ya kisiasa ya ndani ya Iraq, Rais wa Marekani, Joe Biden, na Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iraq, Mustafa Al-Kadhimi, walisaini makubaliano

katikati ya majira ya joto ya mwaka 2021 na kuahidi kwamba shughuli za kivita za vikosi vinavyoongozwa na Marekani nchini Iraq zitahitimishwa rasmi kabla ya kumalizika mwaka 2021.

Mustafa al Kadhimi (kulia) na Joe Biden

Mnamo mwaka 2020, katika mwaka wa mwisho wa urais wa Donald Trump, Marekani ilipunguza idadi ya askari wake walioko Iraq hadi 2,500. Kidhahiri, kazi za vikosi vya jeshi la Marekani nchini Iraq zilikamilika Desemba 31, 2021. Lakini pamoja na hayo, Washington ingali inaendelea kuwepo kijeshi katika nchi hiyo kwa anuani nyinginezo na ina kambi kadhaa za kijeshi huko Iraq ikiwemo ya A'inul-Asad katika mkoa wa Al-Anbar na kambi ya Harir mkoani Erbil.

Licha ya mpango uliopitishwa na Bunge la Iraq wa kutaka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo, Washington ingali imepiga kambi nchini Iraq kwa kisingizio cha kutoa ushauri na mafunzo ya kijeshi, suala ambalo limekabiliwa na mijibizo mikali ya Wairaqi na jibu la utumiaji nguvu, ambalo ni kushuhudiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi hiyo na Syria.

Mashambulizi hayo yamepamba moto zaidi hasa baada ya kuanza hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kufuatia Operesheni ya Oktoba 7 ya Kimbunga cha Al-Aqsa.

Sababu ya mashambulizi hayo, ambayo yamekuwa yakilenga vituo vya Marekani nchini Iraq na Syria kwa kutumia maroketi, makombora na ndege zisizo na rubani, ni kuhusika Marekani hiyo katika kuiunga mkono na kuisaidia waziwazi Tel Aviv kisiasa na kwa silaha na kutumiwa silaha hizo za Washington kuulia wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza. Muqawama wa Iraq, nao pia ukienda sambamba na matakwa ya wananchi wa Iraq, unataka kuwepo kijeshi Marekani katika nchi hiyo kukomeshwe haraka iwezekanavyo.

Katika kukabiliana na hatua hizo, Washington imetoa mjibizo kwa kufanya mashambulio kadhaa dhidi ya makundi ya Muqawama ya Iraq. Baada ya shambulio la hivi karibuni la ndege za Marekani dhidi ya makao mawili ya Al-Hashdu-Shaabi, ambalo lilipelekea kuuawa shahidi wanachama wawili wa harakati hiyo, serikali ya Iraq ilitoa taarifa kulaani shambulio hilo na kutangaza kuwa itaishtaki Washington, ikiwa ni kutetea mamlaka ya utawala wa Iraq katika ngazi ya kimataifa. Sambamba na kulaani shambulizi la jeshi la Marekani kwenye makao ya Al-Hashdu-Shaabi, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq Qasim al-Aaraji amesema, shambulio hilo ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi yake.

Suala muhimu ni kwamba madai ya Marekani kuhusu nia yake ya kujiondoa kijeshi Iraq yametiliwa shaka na muqawama wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, sambamba na kuwepo minong'ono ya kufanyika mazungumzo kati ya Marekani na Iraq ya kuhitimisha kuwepo kijeshi Washington nchini humo, Kataaeb Hizbullah imesema, madai ya Marekani ya kuondoka Iraq ni ya hila na hadaa tu, na kwa sababu hiyo imesisitiza kuwa itaendeleza mashambulizi dhidi ya wavamizi hao hadi pale watakapoondoka kikamilifu katika ardhi ya Iraq. Katika ujumbe kwa wavamizi wa Kimarekani, Abu al-Askari, mkuu wa usalama wa harakati ya muqawama ya Kataaeb Hizbullaq ya Iraq ameionya Washington kwamba "mashambulizi dhidi ya wavamizi wa Kimarekani yataendelea hadi wanajeshi wa nchi hiyo watakapoondoka kikamilifu katika ardhi ya Iraq".../

 

 

 

 

 

 

Tags