Netanyahu apinga pendekezo la kufikia makubaliano na HAMAS
Waziri Mkuu wa Israel amepuuzilia mbali pendekezo la mashirika ya kijasusi ya Mossad na Shin Bet ya utawala huo wa Kizayuni juu ya kufikia mapatano ya kubadilishana wafungwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS).
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina la SAMA, Benjamin Netanyahu amepinga mpango wa kuafikiana na HAMAS kuhusu kubadilishana mateka wa pande mbili.
Baada ya kufanyika duru mpya ya mazungumzo ya usitishaji vita mjini Cairo, vyombo vya habari vya Israel vimedai kuwa Netanyahu amekataa kata kata kuunga mkono pendekezo la jeshi na mashirika ya kijasusi ya utawala huo wa Kizayuni, juu ya kufikia mapatano ya kubadilishana wafungwa na Harakati ya HAMAS.
Vyombo hivyo vya Kizayuni jana usiku viliripoti kuwa, ujumbe wa Israel ukiongozwa na mkuu wa Mossad umeondoka Cairo, mji mkuu wa Misri pasi na kuwepo dalili zozote za kupiga hatua mazungumzo baina yao na wajumbe wa HAMAS.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani Waziri Mkuu wa Qatar aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Doha akiwa pamoja na Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwamba, HAMAS imetoa "jibu chanya" kuhusiana na uwezekano wa kufikia usitishaji vita mpya katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka kati yake na utawala wa Israel.
Itakumbukwa kuwa, katika usitishaji vita wa wiki moja uliofikiwa na HAMAS na utawala wa Kizayuni mwezi Novemba mwaka jana karibu nusu ya mateka wa utawala wa Kizayuni waliachiwa huru mkabala wa kuachiwa huru wafungwa wa Palestina 240.
Wapalestina zaidi ya 28,000 wameuliwa shahidi na wengine zaidi ya elfu 68 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita dhidi ya Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana.