"Kuna haja ya kuitetea Gaza katika Hija ya mwaka huu"
Rais wa Chuo cha Da'awa ya Kiislamu cha Lebanon amesema ibada ya Hija ya mwaka huu ina umuhimu wa kipekee wakati huu ambapo Wazayuni wanaendelea kumwaga damu za Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, "Kuna haja ya kuitetea Gaza katika Hija ya mwaka huu."
Sheikh Ahmed Salehat ametoa mwito huo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na shirika la habari la Iran Press na kueleza kuwa, "Ni miezi minane sasa tangu Ukanda wa Gaza ugeuzwe na Israel kuwa uwanja wa umwagaji damu, lakini dunia eti iliyostaarabika, inatazama tu."
Sheikh Salehat amesema "Dunia inaendelea kushuhudia watoto wa Kipalestina na wakazi wa Gaza wakichinjwa, na hii inathibitisha kuwa, Magharibi inaongopa inapodai kuwa inatetea haki za binadamu na za watoto."
Wapalestina 35,091 wameuliwa shahidi na wengine 78,827 wamejeruhiwa tangu jeshi la utawala wa Kizayuni lianzishe mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 7 mwaka jana. Aidha Wapalestina elfu 10 bado wapo chini ya vifusi vya nyumba zilizobomolewa katika mashambulizi hayo.
Mwanachuoni huyo mashuhuri wa Lebanon amebainisha kuwa, mkusanyiko wa Waislamu kwa ajili ya ibada ya Hija ni kufungamana na nguzo ya Uislamu, na Ihram (vazi linalovaliwa na Mahujaji) ni nembo ya uhuru na ubinadamu, na kuongeza kuwa: Kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hasa Gaza katika Hija ya mwaka huu ni jambop la dharura.
Wiki iliyopita pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei alisema, kwa kuzingatia aya za Qur'ani Tukufu na kumbukumbu ya jina lililobarikiwa la Nabii Ibrahim (AS), ibada ya Hija ya mwaka huu inapaswa kuwa zaidi ya Hija ya kila mwaka, na inabidi iwe Hija na kutangazwa kujitenga au kujibari na adui wa Waislamu, Mzayuni mtenda uhalifu na wafuasi wake wa nchi za Marekani, Uingereza na Wamagharibi kwa ujumla.
Kila mwaka katika mwezi wa Dhul Hijjah, Saudi Arabia hukaribisha Waislamu zaidi ya milioni mbili wanaonuia kwenda kutekeleza ibada ya Hija.