Maafisa wa Israel wafanya ziara ya siri huko Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18814-maafisa_wa_israel_wafanya_ziara_ya_siri_huko_imarati
Licha ya Umoja wa Falme za Kiarabu kutokuwa na uhusiano wa kidiplomasia wala kutoutambua utawala haramu wa Israel, lakini maafisa wa ngazi za juu wa utawala huo wa Kizayuni wamefanya safari ya siri mjini Dubai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2016 00:05 UTC
  • Maafisa wa Israel wafanya ziara ya siri huko Imarati

Licha ya Umoja wa Falme za Kiarabu kutokuwa na uhusiano wa kidiplomasia wala kutoutambua utawala haramu wa Israel, lakini maafisa wa ngazi za juu wa utawala huo wa Kizayuni wamefanya safari ya siri mjini Dubai.

Inaarifiwa kuwa, Danny Danon, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa ameongoza ujumbe wa ngazi za juu wa utawala haramu wa Israel huko Imarati na kushiriki katika kongamano la masuala ya maendeleo lililoandaliwa na UN.

Kongamano hilo la Umoja wa Mataifa mjini Dubai lilifanyika kati ya Jumapili ya Oktoba 30 na Alkhamisi wa wiki hii. Habari zinasema kuwa, wajumbe hao wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya safari hiyo kwa siri kubwa wakiwa chini ya ulinzi mkali ili kutopandisha ghadhabu za wananchi wa Imarati.

Bendera za Imarati na Israel

Mapema mwaka huu, Waziri wa Nishati wa utawala haramu wa Israel pia alifanya ziara ya siri na ya kificho huko Imarati. Waziri huyo huyo ambaye ni mtu wa karibu na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu katika masuala ya mradi wa nyuklia wa Iran, naye pia alifanya safari hiyo ya siri chini ya ulinzi mkali.

Ni vyema kukumbusha kuwa, mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2015, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Israel Emmanuel Nahshon alisema kuwa, Tel Aviv karibuni hivi itafungua ubalozi mjini Abu Dhabi, akisisitiza kuwa ni katika mpango wa kufanikisha shughuli za Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidika IRENA.

Kwa sasa Misri na Jordan ndizo nchi pekee za Kiarabu zenye uhusiano wa kidiplomasia na Israel pamoja na kuwa na balozi za utawala huo wa Kizayuni katika nchi hizo.