Feb 16, 2017 04:06 UTC
  • Saudi Arabia yaendelea kufanya mashambulio dhidi ya wananchi wa Yemen

Ndege za kijeshi za Saudi Arabia zimeendelea kufanya mashambulio dhidi ya Yemen ikitumia mabomu yaliyopigwa marufuku ya fosforasi na vishada.

Shirika Rasmi la Habari la Yemen limetangaza kuwa, ndege za kivita za Saudia jana Jumatano zilifanya mashambulio makubwa katika miji kadhaa ya nchi hiyo ikiwemo ya Taiz, al Hudaydah, Ma'rib na al-Hujjah.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mashambulio hayo yamesababisha uharibifu mkubwa. Aidha mji wa Mokha ni miongoni mwa miji iliyoandamwa na mashambulio hayo ya anga ya Saudia, mji ambao katika majuma ya hivi karibuni umeshuhudia jinai kubwa za Saudia dhidi ya wakazi wa mji huo.

Katika upande mwingine mashirika ya kimataifa ya utoaji misaada yameendelea kutoa tahadhari kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili nchi hiyo masikini ya Kiarabu. 

Mabomu ya vishada yaliyopigwa marufuku yanayotumiwa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen

Saudia, kwa kushirikiana na waitifaki wake, ilianzisha hujuma za kila upande dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kukimbilia Saudia.

Hata hivyo licha ya Riyadh kufanya mauaji na uharibifu mkubwa nchini Yemen, imeshindwa kufikia malengo yake nchini humo. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama linakosolewa kwa kutochukua hatua za maana kukomesha mashambulio na jinai za Saudia huko nchini Yemen.

Tags