Saudia yauzingira mji wa Waislamu wa Kishia
Mji mmoja wenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia uko chini ya mzingiro kwa siku ya saba mfululizo huku raia kadhaa wakiuawa na jeshi walipokuwa katika maandamano ya Amani.
Taarifa zinasema kuwa wanajeshi wa Saudia waliuvamia mji wa Awamiyah Mei 10 kwa kutumia magari ya deraya na silaha nzito nzito. Mji huo uko katika Mkoa wa Mashariki huko Saudia na aghalabu ya wakaazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Utawala wa kiimla wa Saudia unasema lengo la kuuvamia mji huo ni kubomoa mtaa wa kale wa Almosara kwa lengo la kujenga majengo mapya eneo hilo.
Wanaharakati wametuma picha katika mitandao ya intaneti zikionyesha mabuldoza yakiwa yameandamana na magari ya deraya ya jeshi la Saudia katika eneo hilo. Wakaazi wa Awamiya wanasema kufuatia mzingiro huo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na umeme.

Tangu lilipoanza vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu mwaka 2011 katika nchi za Kiarabu za eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, nchi nyingi za Kiarabu za eneo hili ikiwemo Saudi Arabia zimekuwa uwanja wa maandamano ya wananchi ya kupinga tawala za nchi hizo.
Nchini Saudia wimbi la maandamano ya upinzani limekuwa likishuhudiwa zaidi katika maeneo ya Waislamu wa Kishia mashariki mwa nchi hiyo. Utawala wa Aal-Saud umetumia mkono wa chuma kuzima maandamano hayo ya wananchi ambapo hadi sasa mamia ya watu wameuliwa au kufungwa gerezani.