Hizbullah: Inashangaza kuona waungaji mkono wa ugaidi wakiuhusisha muqawama na ugaidi
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon katika eneo la Beqaa amesema kuwa, anashangazwa na Marekani kuutuhumu muqawama na ugaidi katika hali ambayo ni nchi hiyo ndiyo inayouunga mkono ugaidi wa utawala haramu wa Israel.
Mohammad Yaghi, kiongozi wa Hizbullah na kamanda wa harakati hiyo katika eneo la Beqaa sambamba na kutoa mkono wa kheri kwa kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu wote duniani amesema kuwa, ni muda sasa ambapo muqawama umekuwa ukituhumiwa kwa ugaidi na maadui na kwamba hili linatokana na harakati hiyo kusimama imara katika kukabiliana na adui Mzayuni.
Sambamba na kuashiria juu ya tuhuma zisizo na msingi za waungaji mkono wa ugaidi hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, afisa huyo amesema kuwa, tuhuma hizo haziwezi kubadili ukweli wa mambo na kwamba msimamo wa Washington kuuhusu muqawama sio jambo jipya. Amesema kuwa, tangu mwaka 1982 kulipoundwa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah, Marekani imekuwa ni adui nambari moja wa muqawama huo. Mohammad Yaghi pia ametoa pongezi za kumbukumbu za ushindi wa mwaka 2000 za kufurushwa utawala wa Kizayuni kutoka katika ardhi za kusini mwa Lebanon, baada ya askari wa Israel kushindwa vibaya na wanamapambano wa Hizbullah na kuongeza kuwa, ushindi huo ulitokana na juhudi za wanamuqawama, kujitolea nafsi zao na kusimama imara kwa ajili ya taifa la Lebanon.
Kabla ya hapo Sheikh Hassan Baghdadi, mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah nchini Lebanon alinukuliwa akisema kuwa, kuondolewa wavamizi wa Kizayuni katika ardhi za Lebanon hapo mwaka 2000, kulitokana na vita vya kihistoria dhidi ya adui huko Mzayuni. Ushindi wa muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon ulifikia kilele tarehe 25 Mei 2000 kwa kuhitimisha ukaliaji mabavu wa Israel wa miaka 22 katika eneo la kusini mwa Lebanon.