Netanyahu atoa wito wa kuvunjwa UNRWA
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i30350-netanyahu_atoa_wito_wa_kuvunjwa_unrwa
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa wito wa kuvunjwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA), linalowasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2017 22:53 UTC
  • Netanyahu atoa wito wa kuvunjwa UNRWA

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa wito wa kuvunjwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA), linalowasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina.

Katika mkutano wa baraza la mawaziri hapo jana, Benjamin Netanyahu aliituhumu UNRWA kuwa inaendesha kampeni za chuki dhidi ya Israel, zikiwemo shule zinazofadhiliwa na kuendeshwa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Netanyahu amesema wakati umefika wa kulivunja Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) na kuliunganisha na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Waziri Mkuu wa utawala pandikizi wa Israel amesema tayari amemuandikia barua Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kuhusu pendekezo lake hilo, akisisitiza kuwa UNRWA imechochea mgogoro wa wakimbizi wa Kipalestina badala ya kuupatia ufumbuzi.

Makao makuu ya UNRWA, Gaza

Wakati huo huo, Adnan Abu Hasna, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza amekosoa matamshi hayo ya Netanyahu na kusisitiza kuwa ni ya kipumbavu.

Naye Chris Gunness, Mkuu wa  Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa amesema uamuzi wa kuvunjwa au kubadilishwa majukumu ya UNRWA unaweza kupasishwa tu na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa wingi wa kura.