Wanajeshi wa Saudia wamuua mkuu wa Baraza la Qur'ani huko Qatif
(last modified Sun, 25 Jun 2017 15:28:34 GMT )
Jun 25, 2017 15:28 UTC
  • Wanajeshi wa Saudia wamuua mkuu wa Baraza la Qur'ani huko Qatif

Wanajeshi wa utawala wa Saudi Arabia wamempiga risasi na kumuua mwenyekiti wa baraza la Qur'ani katika mji Awamiya katika eneo la Qatif mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Kanali ya Televisheni ya Nabaa, tukio hilo lilijiri Jumamosi usiku wakati wanajeshi walipofyatulia risasi gari la Amin al Hani akiwa analiendesha katika mji wa Awamiyah ulio eneo la Qatif lenye wakaazi wengi Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya gari hilo kufyatuliwa risasi liliteketea moto na baadaye mwili wa marehemu al Hani ulipatikana ndani ya gari hilo.

Video ya tukio hilo imeenea katika mitandao ya kijamii na kuibua hasira ya wakaazi wa eneo hilo.

Mei 10 wanajeshi wa Saudi Arabia walivamia mtaa wa Al Masourah mjini Awamiyah mashariki mwa nchi hiyo ambapo tokea wakati huo wamewaua watu kadhaa na  kuteteteza moto misikiti, nyumba za raia na shule katika mtaa huo.

Watawala wa Saudia wanataka kuubomoa mtaa wa al-Masourah ambako ndiko alikozaliwa Sheikh Nimri Baqir an-Nimr, mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa Kishia aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na utawala huo mwaka jana. Watawala hao wa Saudia wameuvamia mtaa huo kwa madai ya kuukarabati.

Hivi sasa mtaa wa Al Masourah unafahamika kama nembo ya malalamiko huko mashariki mwa Saudia dhidi ya watawala wa nchi hiyo ya kidikteta. Wataalamu wa masuala ya turathi katika Umoja wa Mataifa wameutaka utawala wa Saudia usitishe mpango wake wa kuubomoa mtaa huo wakisema ni wa kale na ni turathi ya utamaduni na ustaarabu wa eneo hilo