Mahakama ya Saudia yamhukumu kifo mwanaharakati wa Kiislamu
(last modified Sat, 12 Aug 2017 02:22:38 GMT )
Aug 12, 2017 02:22 UTC
  • Mahakama ya Saudia yamhukumu kifo mwanaharakati wa Kiislamu

Mahakama ya Saudi Arabia imetoa hukumu ya kifo kwa mwanaharakati wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia anayepinga sera za utawala wa kifalme wa nchi hiyo huku serikali ya Riyadh ikiendelea kuwakandamiza wafuasi wa madhehebu hiyo, wapinzani wa kisiasa na watetezi wa demokrasia.

Mahakama ya Jinai ya Riyadh imetoa hukumu hiyo leo dhidi ya mwanaharakati Haider Al Lif.

Waharakati wa kutetea haki za binadamu wa Saudi Arabia wamelaani hukumu huyo ya kifo na kusema kuwa, watakata rufa ya kuipinga.

Hukumu hiyo ya kifo dhidi ya mwanaharati wa kutetea demokrasia wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia imetolewa siku moja tu baada ya mahakama hiyo hiyo ya Saudia kumhukumu mwanazuoni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Ayatullah Sheikh Hussein al-Radhi kifungo cha miaka 13 jela.

Sheikh al Radhi alitiwa nguvuni tarehe 21 Machi mwaka 2016 baada ya kuzingirwa na askari pamoja na wanamgambo wa Saudia katikati ya mji wa al-Umran.

Ayatullah Sheikh Hussein al-Radhi

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Shia wa Saudi Arabia amekuwa akisumbuliwa kwa ukandamizaji wa aina mbalimbali na kusailiwa ba vyombo vya dola kutokana na hotuba zake za Swala ya Ijumaa ambazo zimekuwa zikizungumzia masuala mbalimbali ya kieneno na ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na hotuba zake zilizokosoa mauaji ya msomi mashuhuri wa nchi hiyo, Sheikh Nimr Baqir al-Nimr mwezi January 2016.

Sheikh al Radhi pia amelaani uvamizi na mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya Waislamu wa Yemen na kuitaka nchi hiyo kuondoa majeshi yake katika nchi jirani ya Yemen.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeutaka utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia kukomesha jinai na mashambulio dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mashariki mwa nchi hiyo.

Eneo la mashariki mwa Saudia lenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaobaguliwa na kukandamizwa limekuwa likishuhudia malalamiko ya wananchi wanaodai usawa na uadilifu tangu mwaka 2011.