Marekani yaiuzia Saudia mfumo wa kujilinda na makombora wa THAAD
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha habari kwamba Washington imeiuzia Saudi Arabia mfumo wa THAAD wa kujilinda na mashambulizi ya makombora.
Shirika la habari la Ufaransa limeinukuu wizara ya mambo ya nje ya Marekani ikithibitisha habari hiyo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, Saudi Arabia imenunua mfumo huo wa THAAD kwa dola bilioni 15.
Wizara hiyo imedai kuwa, hatua ya Marekani ya kuiuzia Saudi Arabia mfumo wa THAAD wa kujilinda na mashambulizi ya makombora imechukuliwa katika kalibu ya usalama wa taifa na siasa za kigeni za Marekani na eti ni katika kuunga mkono juhudi za kuleta usalama wa muda mrefu wa Saudia na eneo la Ghuba ya Uajemi.
Marekani imeiuzia Saudi Arabia mfumo huo wa THAAD kwa madai ya kuudhaminia utawala wa Aal Saud usalama wake katika hali ambayo, Riyadh ni mnunuzi mkuu na wa kudumu wa silaha za Marekani.
Mabilioni ya dola yanayomiminwa na Saudi Arabia ndani ya mfuko wa serikali ya Donald Trump, yanatumika kumuimarisha rais huyo wa Marekani ambaye anatangaza waziwazi chuki zake dhidi ya Waislamu.
Si hayo tu, lakini pia siasa za Marekani na vibaraka wake za kuchochoea vitendo vya kigaidi ndiyo sababu kuu ya kuvurugika utulivu na usalama katika eneo hili hasa kwa vile Marekani ndiye muungaji mkono mkuu wa tawala za kidikteta na kiimla za Mashariki ya Kati.